1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa amani ya Mashariki ya Kati unapatikana 2008?

Kalyango Siraj6 Novemba 2008

Ndoto ya George Bush kuhusu Mashariki ya Kati yaonekana haitatimizwa

https://p.dw.com/p/Fob5
Mmoja wa mahandaki ya WaPalestina.Israel yadai kuwa zinatumiwa kusafirisha silaha hadi GazaPicha: picture-alliance/ dpa

Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameanza safari nyingine ya mashariki ya kati yenye nia ya kufufua mazungumzo ya kuleta amani kati ya Palestina na Israel.

Kuna wanaosema kuwa amekuja kujaribu kuweka mipango ya kuendeleza mazungumzo hayo hapo mwakani kwani pande zote husika zinakubali kuwa mapatano ya amani hayawezi kupatikana mwaka huu.

Masuala mengi yanaonekana kama yamezamisha ndoto ya rais wa Marekani George W.Bush ya kupatikana amani mwaka huu ili kukomesha mgogoro ambao umeendelea kwa miongo sita.

Baadhi ya hayo ni uamuzi wa Israel kufanya uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi mitatu. Ukiongeza ushindi wa Barack Obama, yote haya yanaufanya uongozi wa Bush kuwa na ushawishi mdogo wakati huu ambapo muda wa utawala wake unazidi kuyoyoma.

Maafisa wa serikali ya Marekani wamesema kuwa Bi Condoleezza Rice akiwa katika ziara ya siku nne katika eneo la mashariki ya kati, hana nia ya kutoa mapendekezo yake mwenyewe ili kufanikisha muafaka wa dakika za mwisho.Badala yake waziri huyo wa Marekani atajaribu kufanya walichoita 'kuandaa juhudi mpya' za serikali ya Israel itakayochukua ofisi baada ya uchaguzi wa wabunge utakaofanyika Febuari 10, na vilevile utawala wa Obama utakaoingia ofisini Januari 20.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Sean McCormack amewambia maripota kuwa watajaribu kuweka mchakato wa mazungumzo ya amani katika hali nzuri ili kuwezesha yeyote atakaekuja baadae anaweza kuja na sera zake,na labda anaweza akafuata njia hizo na kuuendeleza akitaka.

Alipoulizwa kama hii ni ishara kuwa Bush ameshindwa katika shabaha yake ya kupata mkataba wa amani mwaka huu,afisa moja wa Marekani ambae hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa inaelekea hivyo.

Na Bi Condoleeza Rice punde tu baada ya kuwasili katika eneo la mashariki ya kati ameonekana kama kukiri kuwa huenda mkataba wa amani, kati ya Isreal na Palestina, usipatikane mwaka huu.Hata hivyo alipowasili Israel amesema kuwa anaamini kuwa ni jambo muhimu kuendeleza mchakato huo na kuunga mkono majadiliano.

Licha ya mazungumzo kadhaa kufanywa kati ya Israel na Palestina lakini hakujaonekana maendeleo ya kimsingi ha sa kuhusiana masuala nyeti. Masuala hayo nyeti ni majaliwa ya mji wa Jerusalem pamoja na ya wakimbizi wa Kipalestina.

Mshauri wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel , amesema kuwa mapema wiki hii,Livni amlimwambia mwanadiplomasia mmoja wa Marekani anaehusika na masuala ya Mashariki ya Kati,David Welch, kuwa mchakato wa amani ni lazima uendelezwe,lakini akaongeza kuwa Marekani isitarajie Israel kuchukua alichoita -njia za mkato- ili kupata mkataba wa amani.

Na hali ikiwa hivyo Condeleezza Rice anapanga kukutana na maafisa wa Israel pamoja na wa Palestina.Pia anatazamiwa kufika katika mji wa Misri wa Sham el-Sheikh ambako kutafanyika mkutano wa wadau wa amani ya Mashariki y kati ambao ni Umoja wa Ulaya,Urusi,Umoja wa Mataifa, pamoja na Marekani.