1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Elysée mfano wa kuigwa ulimwenguni

22 Januari 2013

Ujerumani na Ufaransa zilizowahi kupigana vita mara kadhaa huko nyuma sasa zimegeuka kuwa mfano wa kuigwa duniani kwa sababu ya kuingia kwao kwenye makubaliano maarufu ya Elysée yanayotimia sasa miaka 50.

https://p.dw.com/p/17Oms
Rais Charles de Gaule wa Ufaransa (kulia) na kansela wa wakati ule wa Ujerumani Konrad AdenauerPicha: Getty Images

Ujerumani na Ufaransa zinasherehekea miaka 50 tangu ulipotiwa saini mkataba wa urafiki, mashuhuri kwa jina la "Mkataba wa Elysée" mjini Paris. Sherehe za kuadhimisha mkataba huo, unaoangaliwa kama mfano mwema wa kufuatwa katika nchi zinazokumbwa na mizozo, zinaendelea hivi sasa mjini Berlin kwa kufanyika vikao vya mabaraza ya mawaziri wa nchi hizi mbili, pamoja na vile vya wabunge wa mahasimu hawa wa jadi wa zamani.

Mkataba wa Elysée unasifiwa kuwa kipeo cha historia ya nchi hizi mbili. Makubaliano yaliyofikiwa katika kasri la Elysée ya kujongeleana Ujerumani na Ufaransa, yamechangia pakubwa kuwafanya maadui wakubwa wa zamani wageuke kuwa washirika muhimu kabisa barani Ulaya wakiendeleza maingiliano kujadiliana masuala muhimu kuhusu siasa ya nje, usalama, vijana na utamaduni.

"Suluhu hiyo inapewa umuhimu mkubwa kwa sababu ni ushahidi kwamba Ulaya inaweza kuishi kwa amani," anasema muasisi wa jarida liitwalo "Dokument" linalohimiza mdahalo kati ya Ufaransa na Ujerumani.

"Mapema katika miaka ya 60, bado kulikuwa na watu waliokuwa wakizungumzia kuhusu maadui. Na ilikuwa muhimu sana kuona kwamba angalao madola mawili yenye wakaazi wengi zaidi barani Ulaya yanajikuta katika hali ya kutozungumzia tena kuhusu uadui na badala yake wanazungumzia kuhusu urafiki na ushirikiano." Anasema Gérard Foussier kuhusu umuhimu wa mkataba wa Elysée.

Mfano mzuri wa kuigwa

Stefan Seidendorf Deutsch-Französisches Institut Ludwigsburg
Stefan Seidendorf wa taasisi ya uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa huko LudwigsburgPicha: dfi

Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa unaangaliwa kuwa ni mfano mwema wa kuigwa. Mataifa mengine ya Ulaya na hasa mataifa jirani yenye historia ya malumbano daima yamekuwa yakijikumbusha "mfano mzuri wa kuigwa" wa mkataba wa suluhu kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Mada hiyo hiyo inachambuliwa katika kitabu kilichochapishwa na Stefan Seidendorf wa taasisi ya Ujerumani na Ufaransa mjini Ludwigsburg. Kitabu hicho kilichopewa jina "Uhusiano wa Ujerumani na Ufaransa mfano wa kuigwa" kinazungumzia sababu zinazoweza kujitokeza pia katika mizozo ya nchi nyengine na pia katika uhusiano wa pande mbili.

Seidendorf anazungumzia kifungu cha mkataba wa Elysée kuhusu mikutano ya mara kwa mara inayowaleta pamoja wawakilishi wa kisiasa wa daraja tofauti.

"Hakuna hata mmoja kati ya wawakilishi hao anayeweza kukwepa kushiriki katika mkutano kama huo na kwa namna hiyo mkutano huo hadi hii leo unapewa umuhimu mkubwa hasa wakati wa mizozo pale ambapo watu wangependelea pengine wasionane au kila mmoja angependelea kufuata njia yake." Anasema Seidendorf.

Matumaini kwa vijana

Bildergalerie AGEFA Deutsch-französischer Kindergarten Paris
Watoto katika shule ya chekechea ya Ujerumani na Ufaransa mjini ParisPicha: DW/M. Stegemann

Katika mkataba wa Elysée kuna kifungu kinachozungumzia kuhusu "wakala wa vijana" wa Ujerumani na Ufaransa ulioanzishwa Julai 5 mwaka huo huo wa 1963. Wakala huo umerahisisha vijana wa nchi hizi mbili kukutana mara kwa mara. Vijana milioni nane kutoka nchi hizi mbili wameshashiriki katika maandalizi zaidi ya 300,000 pakifanyika mijadala pamoja na kubadilishana maoni.

Mwandishi: Ralf Bosen/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo