1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zenye silaha za Nyuklia zakataa kuuridhia mkataba huo

Saumu Mwasimba
20 Septemba 2017

Nchi 51 zimesaini makubaliano mapya ya kupinga matumizi ya silaha za nyuklia duniani ambayo yamepingwa vikali na Marekani na nchi nyingine zenye nguvu duniani.

https://p.dw.com/p/2kOQc
USA UN Vollversammlung in New York Antonio Guterres
Picha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Kusainiwa mkataba huu mpya kunajitokeza katika wakati ambapo mgogoro kuhusu Korea Kaskazini ukizidi kufukuta. Kadhalika hatua hii ya kusaini mkataba huo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutishia kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini pale nchi yake itakapolazimika kujilinda au kuwalinda washirika wake.

Mkataba unaopinga kutumika kwa silaha za maangamizi makubwa uliidhinishwa na nchi 122 katika Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Julai baada ya kufanyika majadiliano ya kina yaliyoongozwa na Austria, Brazil, Mexico, Afrika Kusini na New Zealand. Hakuna nchi hata moja kati ya tisa zinazomiliki silaha hizo za nyuklia iliyoshiriki katika mazungumzo hayo, zikiwemo Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Uingereza, India, Pakistan, Korea Kaskazini na Israel, ambayo haijawahi kukiri hadharani ingawa inafahamika kuwa nazo.

Nchi hizo zenye kumiliki silaha hatari kabisa duniani zinahoji kwamba zana zao hizo zipo kwa ajili ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kinyuklia na kwamba zimejitolea katika kuuzingatia mkataba unaokataza uenezaji wa silaha hizo unaofahamika kama Non-Proliferation Treaty, NPT.

President Trump UN Diskussion
Picha: Getty Images/C.Ochs

Leo hii,(20.09.2017) Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefungua rasmi sherehe za kuutia saini mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha hizo za nyuklia katika Umoja wa Mataifa akisema kwamba ni msingi uliofikiwa na nchi nyingi katika kuunga mkono kuzuia matumizi ya silaha hizo katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.

''Mkataba juu ya kuzuia kueneza sialaha za nyuklia ni matokeo ya kuongezeka wasiwasi kuhusiana na kitisho kinacholetwa na kuendelea kuwepo kwa silaha za Nyuklia ikiwemo majanga ya kibinadamu na athari za kimazingira kutokana na kutumika silaha hizo.Mkataba huu ni hatua muhimu kuenelea lengola  ulimwengu usiokuwa na silaha za maangamizi na ni matumaini yake kwamba mkataba huu utachochea juhudi za ulimwengu kulifikia lengo hili''

Hata hivyo, Guterres amekiri pia kwamba hatua zaidi zinahitajika ili kuondokana na mrundikano wa makombora 15,000 ya kufyetuwa mabomu ya atomiki. Mkataba huo utaanza kutekelezwa baada ya nchi 50 kuuidhinisha.

Korea Kaskazini imechochea ulimwengu kuwa katika hali ya mashaka baada ya kuonekana kuendelea  kufyetua makombora yake ya nyuklia.

USA UN Vollversammlung in New York
Picha: picture-alliance/Photoshot/W. Ying

Hata hivyo, Marekani, Uingereza na Ufaransa zimeupuuzilia mbali mkataba huo na kusema kwamba hauzingatii hali halisi ya ulimwengu ulivyo. Nchi hizo zenye nguvu ya nyuklia zinasema marufuku ya silaha haiwezi kusaidia kitu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean Yves Le Drian, amesema mkataba huo haukaribiani na uhalisia.

Mkataba huo wa NPT uliopatikana kipindi cha miongo kadhaa unataka kutafuta njia za kuzuia kuenea kwa silaha za atomiki lakini pia unazitaka nchi ambazo tayari zinamiliki silaha hizo kupunguza mrundikano wa silaha walizonazo.

Wasiwasi unaendelea kuongezeka miongoni mwa nchi ambazo hazimiliki silaha hizo kuhusiana na kasi ndogo ya kumalizwa kwa silaha hizo, huku kukiweko mashaka kwamba silaha za maangamizi makubwa huenda zikaingia mikononi mwa mikono ya watu hatari.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef