1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa Schengen huenda ukasimamishwa kwa muda

26 Januari 2016

Umoja wa Ulaya unasema mkataba wa eneo la Schengen, huenda ukasimamishwa kwa hadi miaka miwili ikiwa utashindwa katika wiki chache zijazo kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika

https://p.dw.com/p/1HjuS
Deutschland Grenzkontrollen an der Grenze zu Österreich
Picha: Getty Images/AFP/G. Schiffmann

Utekelezwaji wa muda mfupi wa udhibiti wa mipaka ya eneo hilo utakamilika mwezi Mei. Mawaziri wa uhamiaji wa serikali za Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Amesterdam wameamua kuwa mipaka huru ya Schengen huenda ikaendelea kudhibitiwa kwa miaka miwili – hatua ya kurefushwa ambayo haikutarajiwa – kwa sababu mzozo wa uhamiaji huenda usiweze kudhibitiwa ifikapo wakati huo, kwa mujibu wa waziri wa uhamiaji wa Uholanzi, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Baadhi ya mawaziri walieleza wazi kuwa hatua ya aina hiyo ya muda mfupi kinadharia inaweza kuitenga Ugiriki, ambako zaidi ya watu 40,000 wamewasili kupitia baharini wakitoka Uturuki, licha ya makubaliano na serikali ya Uturuki miezi miwili iliyopita yaliyoitaka izuie mmiminiko wa wakimbizi wa Syria. Zaidi ya watu 60 wamekufa majini tangu Januari mosi mwaka huu.

Tagung der EU-Innenminister in Amsterdam über den Grenzschutz in der Flüchtlingskrise
Lakini waziri wa Uhamiaji wa Uholanzi, Klaas DijkhoffPicha: Getty Images/AFP/R. van Lonkhuijsen

Maafisa wa Ugiriki wamesema kuwa kufungwa njia hizo zinazotumiwa na wahamiaji, hakuwezi kutatua tatizo hilo. Lakini shinikizo la wananchi kwa serikali zao, ikiwa ni pamoja na nchi yenye nguvu kubwa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya, Ujerumani, kudhibiti na kupinga juhudi za kuwasambaza waomba hifadhi kote katika umoja huo zinafanya sheria za usafiri huria kutozingatiwa.

Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos amezitaka nchi wanachama kuzitekeleza hatua walizokubaliana kwa kudhibiti uhamiaji kote barani huo – la sivyo mkataba wa eneo la Schengen uliodumu miaka 30 utaporomoka.

Lakini waziri wa Uholanzi, Klaas Dijkhoff anasema muda umekwisha wa kuendelea kuutekeleza mfumo huo ambao umewaruhusu mamia kwa maelfu ya watu kutembea kwa miguu kutoka Ugiriki na Italia na kuingia Ujerumani na Sweden katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kansela wa Ujeruamani Angela Merkel, ambaye aliifungua mipaka ya nchi yake kwa wakimbizi wan Syria, ana anakumbwa na shinikizo kubwa la kumtaka asitishe mmiminiko huo, baada ya zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia Ujerumani mwaka jana.

Umoja wa Ulaya umechukua hatua kadhaa za kuipa Ugiriki inayokabiliwa na mgogoro wa kifedha, msaada wa kifedha ili kukabiliana na mzozo wa wahamiaji, lakini mataifa mengi wanachama wanaamini kuwa Athens haifanyi vya kutosha. Umoja wa Ulaya sasa umependekeza kuzinduliwa kwa kikosi cha pamoja cha walinzi wa pwani na mipaka ya Ulaya ili kuimarisha udhibiti wa mipaka ya Umoja huo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo