1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wayoyoma katika mazungumzo ya mkopo kwa Ugiriki

25 Juni 2015

Mazungumzo mapya yameanza kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake, huku muda ukizidi kuyoyoma, na pande hizo zikiwa bado zinatofautiana kuhusu mageuzi katika sekta muhimu za kodi, malipo ya uzeeni na ajira.

https://p.dw.com/p/1Fn6o
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras amekataa kuridhia shinikizo la wakopeshaji wa nchi yake
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras amekataa kuridhia shinikizo la wakopeshaji wa nchi yakePicha: Reuters/P. Hanna

Waziri Mkuu wa Ugiriki anakutana tena na viongozi Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na wa Shirika la Fedha Ulimwenguni - IMF, baada ya kukataa hapo jana mageuzi yanayopendekezwa na wakopeshaji wa nchi yake.

Kwa pamoja watajaribu kupata makubaliano haraka, ili yaweze baadaye leo kuidhinishwa na mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro ambao watakutana baadaye leo, ili hatimaye yapitishwe na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kufanyika leo na kesho.

Kadri muda wa mwisho kwa Ugiriki kulipa madeni yake, tarehe 30 mwezi huu wa Juni unavyozidi kukaribia, mazungumzo yanaghubikwa na jazba, na jana Ugiriki iliondoa baadhi ya mapendekezo yake, hiyo ikiwa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mazungumzo hayo.

Ugiriki yakataa kulegeza kamba

Baadhi ya mapendekezo yaliyoondolewa kwenye meza ya mazungumzo, hii ikiwa kwa mujibu wa chanzo cha habari katika serikali ya Ugiriki, ni yale yanayohusu kupandisha mchango kwa ajili ya akiba ya uzeeni, ambayo yanachukiwa sana nchini Ugiriki.

Rais wa IMF, Christine Lagarde (kulia katika picha)
Rais wa IMF, Christine Lagarde (kulia katika picha)Picha: Reuters/P. Wojazer

Hata hivyo, chanzo kingine kutoka Umoja wa Ulaya kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba yapo matumaini ya kupatikana maelewano katika mkutano huo baina ya waziri mkuu Tsipras na viongozi wa Halmashauri ya Ulaya na wa IMF.

Wakati huo huo mawaziri wa fedha wa nchi 19 wanachama wa kanda inayotumia sarafu ya Euro, watajadili uwezekano wa kuachia awamu nyingine ya mkopo kwa Ugiriki mchana wa leo, baada ya kushindwa kuelewana katika mkutano wao jana usiku ambao ulidumu kwa saa moja tu.

Bado matumaini hayajapotea

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mkutano huo jana usiku, mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa fedha wa kanda ya euro Jeroen Dijsselbloem alisema wataendelea na kazi.

Mwenyekiti wa mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro, Jeroen Dijsselbloem
Mwenyekiti wa mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro, Jeroen DijsselbloemPicha: J. Thys/AFP/Getty Images

''Kwa bahati mbaya hatukupata makubaliano, lakini tunaazimia kuendelea kuyafanyia kazi, na ikiwa lazima kazi itaendelea hadi usiku. Tutakutana kesho saa saba mchana, kufanya tathmini ya hatua iliyopigwa''. Amesema Dijsselbloem.

Baada ya kukwama kwa mazungumzo hayo mjini Brussels jana, waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras aliwashambulia vikali wakopeshaji wa nchi yake, kutokana na kile alichosema ni masharti yaliyoongezwa juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na nchi yake wiki iliyopita.

''Msimamo huu wa ajabu unaweza kuwa unaficha mambo mawili'', amesema Tsipras na kuongeza, ''Ama hawataki kabisa makubaliano yafikiwe, au wanatumikia maslahi fulani ya kisiasa nchini Ugiriki'', alimalizia kiongozi huyo.

Maafisa wanasema mazungumzo haya yanaweza kuendelea kwa muda wa saa 48 zijazo, lakini ikiwa hakuna makubaliano yatakayopatikana kufikia Jumamosi, Ugiriki inaweza kukosa fedha inazohitaji kulipa deni la IMF kabla ya muda wa mwisho uliowekwa.

Mwandishi:Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo