1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkosoaji wa serikali ya Rwanda Paul Rusesabagina akamatwa

31 Agosti 2020

Mkosoaji wa Serikali ya Rwanda anayeaminika kuwa na makazi Ubelgiji na Marekani, Paul Rusesabagina, amekamatwa na kurudishwa nchini Rwanda na kuoneshwa mbele ya vyombo vya habari mjini Kigali.

https://p.dw.com/p/3hoY3
Ruanda Paul Rusesabagina
Picha: Imago Images/Belga/M. Maeterlinck

Kitengo cha kufuatilia wahalifu kimesema anatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi na utekaji vilivyofanywa mwaka 2018 dhidi ya raia Kusini mwa Rwanda. 

Akiwa amevaa suti nyeusi, shati nyeupe, tai ya njano na barakoa ya rangi ya bluu, Bwana Rusesabagina ameoneshwa mbele ya waandishi wa habari katika hatua iliyowashangaza wengi, maana hakuna aliyekuwa na habari za kukamatwa kwake.

Waandishi wa habari walishikwa na butwaa na bumbuazi alipoingia katika chumba walichokuwemo, akiwa ameambatana na askari polisi watatu. Msemaji wa ofisi ya taifa ya upelelezi Dr Thierry Murangira, amesema  Rusesabagina alitiwa mbaroni kwa ushirikiano wa kimataifa.

"Rusesabagina anatuhumiwa kwa kuunda na kuongoza chama cha kigaidi pamoja na mtandao wa vyama vya kigaidi ikiwemo MRCD na PDR-Ihumure ambavyo vina shughuli mbalimbali katika ukanda huu na kwingineko” Amesema Murangira.

"Rusesabagina alikuwa amewekewa waranti wa kimataifa ya kumkamata ili sheria ifuate mkondo wake, ajitetee juu ya makosa makubwa yanayomkabili ikiwemo ugaidi, uchomaji na mauaji yaliyofanywa dhidi ya wananchi wasio na hatia katika mashambulizi yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali nchini Rwanda ikiwemo shambulizi la mwezi juni 2018 huko Nyaruguru na lile la Nyamagabe lililofanyika Disemba 2018.”

Bwana Murangira amejizuia kutoa maelezo kuhusu nchi aliyokuwemo Ruisesabagina wakati anakamatwa, na hata tarehe, akisema utoaji wa taarifa hizo unaweza kupotosha juhudi za upelelezi unaoendelea.

Paul Rusesabagina alipata sifa kemkem kutokana na filamu iliyoitwa Hotel Rwanda
Paul Rusesabagina alipata sifa kemkem kutokana na filamu iliyoitwa Hotel RwandaPicha: picture-alliance/dpa/Tobis Film

Paul Rusesabagina ni mtu maarufu nchini Rwanda na duniani hasa kupitia filamu ya Hotel Rwanda, iliyochezwa juu ya mchango wake katika kuwaokoa mamia ya watutsi waliokimbilia katika Hoteli ya Milles Collines iliyokuwa chini ya uongozi wake mwaka 1994 katika kipindi cha mauaji ya kimbari. Filamu hiyo imemleta tuzo za kimataifa kama mpigania haki huku ikikosolewa na wengine wanaosema imesheheni uongo.

Bwana Rusesabagina mwenye umri wa miaka 66, anatambulika pia kama mkosoaji wa Serikali ya Rwanda. Jina lake limetajwa mara nyingi katika kesi ya Nsabimana Callixte maarufu Sankara, ambaye pia alikamatwa akiwa ugenini na kurudishwa nchini Rwanda mwaka jana akikabiliwa na makosa mengi ikiwemo ugaidi.

Waendesha mashtaka walisema Rusesabagina ndiye aliunda kile walichokitaja kuwa mtandao wa kigaidi wa MRCD ambao tawi lake la kijeshi la FLN lilikiri kufanya mashambulizi Kusini mwa Rwanda mwaka 2018, kwa lengo la kuuangusha utawala wa Rais Paul Kagame ambaye wakosoaji wake wanamtuhumu kutovumilia ukosoaji wa aina yoyote.

Mwandishi: Janvier Popote/DW, Kigali.

Mhariri: Daniel Gakuba