1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano kuhusu dini lafanyika Lindau, Ujerumani

Josephat Charo
22 Agosti 2019

Wawakilishi wa kidini kutoka  kila pembe ya dunia wanaendelea kukutana hadi Agosti 23 katika mji wa Lindau unaopakana na Bodensee, ziwa linalopakana na Ujerumani, Austria na Uswisi.

https://p.dw.com/p/3OJAQ
Lindau Religions for Peace
Picha: DW/C. Papaleo

Rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinemeier, ndiye aliyeufungua mkutano huo wa kumi wa aina yake, uliopewa jina "Dini kwa ajili ya amani," kongamano lililobuniwa tangu mwaka 1970 na kuwakilisha kwa namna moja au nyengine takriban dini zote za dunia. Kuna wanaofika hadi ya kulinganisha na hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, kongamano hilo linaloitishwa mara moja kila baada ya miaka mitano.

Wolfgang Schürer, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi ni mwenyekiti wa taasisi inayohimiza mazungumzo ya amani kati ya dini za dunia na jamii. Akiulizwa na DW kuhusu matarajio yao kuelekea kongamano hilo la "Dini kwa ajili ya amani" Wolfgang Schürer alisema, "Inategemea kwa sehemu kubwa kwa jinsi gani tunawajibika. Matarajio ya aina gani, imani na uvumlivu wa aina gani tunadhihirisha."

"Mengi yatategemea hali hiyo. Matarajio tunayofungamanisha na kongamano hili la kimataifa ni kuona tunachochea kitu kitakachodumu na sio kugeuka kuwa miongoni mwa ile mikutano ya kilele inayoitishwa kila kukicha ulimwenguni," akaongezea kusema.

Matumaini ni makubwa

Matumaini hayo yanalingana na matarajio ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani mjini Berlin iliyochangia mamilioni kadhaa ya euro kuhakikisha mkutano huo wa kimataifa wa Lindau unaitishwa.

Lindau Religion for Peace Religionen für den Frieden
Mji wa Lindau ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa uliopewa jina "Dini kwa ajili ya Amani"Picha: Ahmad Khalid Photography

Sababu mojawapo kubwa ni kwamba katika nchi nyingi za dunia vituo vya kidini vinakamata nafasi ya mashirika ya huduma za jamii; mfano katika vijiji vya Jamahuri ya Afrika Kati, Iraq au katika kambi za wakimbizi katika nchi mbalimbali za dunia. Kwa maneno mengine wanasiasa wanatambua umuhimu na nguvu za jumuiya za kidini na kwa namna hiyo wanataka kuhakikisha zinawajibika pia katika kuimarisha amani.

Kongamano la Lindau linazungumzia pia mada zinazozusha mabishano. Vikao vya siri vinatarajiwa kuitishwa kwa mfano kati ya wawakilishi wa Korea ya Kaskazini na wale wa Korea ya Kusini, Myanmar na Bangladesh na pia kati ya wawakilishi wa Sudan na Sudan Kusini.

Miongoni mwa wanaohudhuria kongamano hilo la Lindau ni pamoja na mwanasiasa mashuhuri wa Timor Mashariki, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Jose Ramos Horta, Layla Alkahafaji, ambaye ni muumini wa dini ya kiislamu wa Iraq aliyewaahi kufungwa miaka kumi wakati wa utawala wa Sadam Hussein kabla ya kukimbilia nchini Canada na kugeuka kuwa mwanaharakati anayepaza sauti kupinga matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake. Au kadinali John Onaiyekan wa Nigeria ambaye licha ya vitisho na mashambulio ya wanamgambo wa itikadi kali Boko Haram, anaendelea kuhimiza mshikamano kati ya waumini wa dini tofauti.

Kwa jumla wawakilishi 900 wa kidini kutoka nchi 100 wanahudhuria kongamano hilo la kimataifa.

(Strack, Christoph)