1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu elimu kwenye mtandao wamalizika Dakar

Charo Josephat29 Mei 2009

Bara la Afrika latakiwa kujitokeza zaidi

https://p.dw.com/p/I0GB
Rais wa Senegal, Abdoulaye WadePicha: PA/dpa

Mkutano wa siku tatu kuhusu elimu kwa njia ya mtandao barani Afrika umemalizika leo mjini Dakar Senegal. Mkutano huo ambao unaelezwa kuwa mkubwa kuwahi kufafanywa barani Afrika kuhusu matumizi ya teknolojia katika elimu, umehudhuriwa na wajumbe 1,300 waliobadilishana uzoefu wao na maoni yao kuhusu teknolojia mpya ya habari na mawasiliano katika elimu na maendeleo.

Mihadhara takriban 300 iliyotolewa na wanasayansi na wataalam wa taaluma ya elimu kupitia njia ya mtandao wa intaneti barani Afrika imelitaka bara la Afrika lijitokeze zaidi uliwemguni katika swala hili. Swala muhimu ni kuvumbua mifumo ya elimu na mafunzo inayoweza kutumika katika bara la Afrika wakati huu. Vipi elimu kupitia mtandao inavyoweza kuchangia katika kukaribia kuyafikia malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa. Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade, katika hotuba yake ya ufunguzi alisema vyuo vikuu vinaweza kutumiwa katika kutoa elimu kupita mtandao.

"Tuna nia kubwa ya kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ajili ya elimu, lakini kwanza tunatakiwa tufanye hivyo kwa maafisa wa elimu. Na hilo ndilo tunalolifanya hapa nchini Senegal. Elimu kupitia mtandao inatolewa katika vyuo vikuu katika ngazi ya juu. "

Tim Unwin, kiongozi wa mawasiliano ya kimaendeleo katika shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, ambaye alishiriki katika kuandaa mkutano wa Dakar, ana maoni tofauti. Kwa mtazamo wake kitu cha kufurahisha kuhusu elimu ya mtandao ni kuunganishwa kwa mitandao na njia zote mpya za elimu, kuunda maswala shirikishi na kuunganisha jamii. Kwake yeye elimu ya mtandao inahusu kubadilishana uzoefu katika kujifunza, kufanya vitu kwa njia mpya kutoka ngazi ya chini kwenda juu. Mkutano wa mjini Dakar umetumiwa kuhamasisha na kuongeza hadhi ya elimu ya mtandao barani Afrika na kuonyesha kinachoweza kufanywa.

Joshua Mallet, mtaalam wa elimu kutoka Ghana anasema simu za mkononi zinaweza kutumiwa katika elimu kwa watu wengi barani Afrika wanamiliki simu hizi hata wale ambao hawajaenda shule. Matumizi ya simu za mkononi katika elimeu ni swala lilijadiliwa kwa mapana na marefu katika mkutano wa mjini Dakar. Hata hivyo sio wajumbe wengi walioshawishika kwamba simu za mkononi zinaweza kutumiwa kuchukua nafasi ya mifumo ya kutoa elimu inayotumiwa hivi sasa, ingawa zimeenea sana barani Afrika kuliko kompyuta. Huyu Tim Unwin, mjumbe wa shirika la UNESCO katika mkutano huo wa Dakar.

"Bado nadhani kuna matumizi duni ya simu za mkononi katika elimu kwa njia ya mtandao. Bado sijashawishika kwamba kuna uelewa wa kutumia simu za mkononi barani Afrika kwa ajili ya manufaa ya jamii maskini kuhusiana na elimu."

Joshua Mallet, mtaalam wa elimu kutoka Ghana, amesema bara la Afrika linatakiwa kutafuta njia yake na kutumia mifumo mbalimbali ya elimu kuhakikisha elimu na maendeleo yanawafikia walengwa wote.

"Barani Afrika tunatakiwa kuzungumzia kuhusu elimu jumla. Iwe ni kwa mtandao kupitia kompyuta, redio ama simu ya mkononi. Nadhani hatutakiwi kugawa makundi na kusema tupo katika enzi ya kujifunza kupitia mtandao au redio za kijamii. Elimu inatakiwa kutolewa kutumia njia mbalimbali kwa pamoja."

Mkutano kuhusu elimu kupitia mtandao uliowaleta pamoja wajumb ekutoka nchi 80 umemalizika mjini Dakar ikibanika wazi kwamba elimu kwa njia ya mtandao si swala la ikiwa linawezekana bali ni vipi linavyoweza kufanywa. Afrika ina jukumu la kubuni mifumo yake inayofaa kutumika kwa wakati huu.

Mwandishi: Sussane Fuchs/ Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraji