1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kujadili matobwe ya Gaza wafanyika Denmark

Charo Josephat 4 Februari 2009

Uingizaji wa bidhaa na silaha kinyume cha sheria waendelea Gaza

https://p.dw.com/p/GnDS
Mpaka kati ya Gaza na Rafah upande wa MisriPicha: AP

Mkutano wa siku mbili unaojadili uingizaji silaha kinyume cha sheria huko Gaza kwa kutokea Misri ,kupitia matobwe au njia za chini kwa chini, unaendelea mjini Coppenhagen nchini Denmark. Mkutano huo ulioanza jana unahudhuriwa na wataalamu kutoka Mashariki ya Kati, Marekani na Ulaya.

Israel inataka matobwe hayo yafungwe kwa kuwa yanatumiwa kuingiza silaha katika Ukanda wa Gaza. Ukweli ni kuwa ili mradi mipaka ya ardhini inabakia kufungwa, kila kitu kinachohitajika Gaza hupitishwa chini kwa chini kupitia matobwe haya, ikiwa ni pamoja na vipuri vya magari, majiko ya mafuta, viatu, nepi au sabuni ya kuoshea nywele.

Soko moja katikati mwa mji wa Gaza, juma moja baada ya vita kusitishwa. Wakulima katika vitongoji vya mji huo wanauza nyanya, viazi, machungwa na matunda, kila kitu kinachopatikana hapa kinatoka maeneo ya mashambani. Kila kitu kitasafirishwa nchi jirani kimagendo kupitia matobwe.

Vipande vitano vya sabuni vinauzwa kwa shekeli kumi ambazo ni takriban yuro mbili. Nchini Misri gharama ya sabuni hii ni nusu ya gharama yake katika Ukanda wa Gaza. Kuchimba tombwe moja hugharimu dola 70,000 za Kimarekani. Fedha hizi wanalazimika wawekezaji kuzirudisha. Wapalestina wengi ambao zamani walifanya kazi nchini Israel, sasa wanafanya kazi ndani ya matobwe haya.

Washirika wenzao wa kibiashara wanaishi upande wa pili wa mpaka wa nusu ya mji wa Rafah inayomikiliwa na Misri. Hawataki kuacha kazi yao ya magendo.

Wanaume wengi katika kitongoji cha Barameh mjini Rafah walihukumiwa vifungo gerezani na mahakama ya kijeshi bila wao kuwepo mahakamani. Wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka kumi jela watakapokamatwa. Hawalali nyumbani na hukwepa vituo vya upekuzi.

Katika majuma yaliyopita maafisa wa polisi wa Ujerumani walikuwa Rafah kuwashauri polisi wa Misri kulinda mpaka. Wakati huu kuna ujumbe wa wataalamu wa Marekani mjini Rafah na ghafla barabara zote zimefungwa, wanasema wafanyabiashara haramu kuwa shinikizo kutoka nje linadhihirisha kuwa na athari.

Kufungwa kwa mpaka kunazifanya siasa za ndani ya Misri kuwa ngumu, kwa kuwa njia za chini ya ardhi zimekuwa vyanzo vikuu vya biashara haramu katika eneo lisiloshughulikiwa la kaskazini mwa Sinai.

''Ikiwa hawataki uingizwaji wa vitu kimagendo katika Ukanda wa Gaza, wanatakiwa waifungue tena mipaka. Halafu hakutakuwa tena na tatizo hilo. Huyu hapa ni dereva wa teksi na huyu pia. Sote tumefanya kazi pamoja mpakani. Huko kulikuwa na teksi takriban 1,200 zikifanya kazi. Zilifanya safari mbili au tatu kwenda na kurudi. Kwa ujumla bila shaka watu 5,000 wamepata riziki kutoka mpakani.''

Watu sasa wanaishi kutokana na njia za chini kwa chini na kwa wengine mambo si mabaya. Kila upande wa mpaka kuna majumba ya kifahari ambayo hayakujengwa kutumia fedha zilizopatikana kwa kuuza chai na keki kimagendo. Wakaazi wa kitongoji cha Barameh wamekiri wameingiza mafuta aina ya diesel kinyume cha sheria na wala sio silaha.

Ni rahisi kupata silaha. Kando ya kiti cha dereva kuna bunduki iliyotengenezwa nchini Urusi. Mwenye bunduki hiyo anasema imegharimu yuro 1,000. Nje ya mji wa Rafah kwenye mashamba ya mizeituni, mtu anaweza pia kukutana na wafanyabiashara haramu ya kuuza silaha wanaosafirisha silaza hizo. Wanafunika nyuso zao na kutaka yuro 1,000 kuzisafirisha kupitia njia za chini kwa chini.

''Biashara hiyo inaendelea na hata mashambulizi ya angani ya ndege za kivita hayawezi kubadili chochote'', anasema mfanyabiashara huyu anayeingiza mafuta ya diesel kinyume cha sheria. Pia ameongeza kusema, ''Ili mradi Ukanda wa Gaza unabakia kufungwa, watu watachimba matobwe hata kama wamefikia kina cha mita 200 chini ya ardhi. Mtu mwenye njaa na anayetaka kula afanye nini?''

Tangu miezi sita iliyopita, Israel imekuwa ikiamua kitu gani kinachotakiwa kuagizwa kutoka nje ya Gaza na kwa kiwango gani. Tangu vita kusitishwa, bidhaa zimekuwa zikiingizwa kupitia mpakani, malori kati ya 70 na 120 kila siku. Kiwango hicho hakitoshi, anasema John Ging, mkurugenzi wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza.

''Inatosha iwapo unaridhika na kuwawezesha watu kuendelea kuwa hai - hai lakini masikini. Leo malori 140 ya misaada yametufikia kwa ajili ya watu milioni 1,5. Miezi 18 iliyopita yalikuwa yakija malori 600 kila siku. Hapo kulikuwa na uwiano kati ya mahitaji na ukweli wa mambo. Juu ya hayo sasa mahitaji yameongezeka mno baada ya vita vya Gaza. Kwa sasa tunapokea takriban asilimia 20 ya mahitaji tunayohitaji hapa.''

Na ili mradi hali itaendelea kuwa hivyo, mji wa Rafah utaendelea kuchimbwa matobwe.