1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa waanza New York

Zainab Aziz19 Septemba 2016

Mkutano utajadili vita vya Syria na mgogoro wa wakimbizi duniani, wakati juhudi za Marekani na Urusi za kusitisha mapigano nchini Syria zikikabiliwa na hali ya wasiwasi.

https://p.dw.com/p/1K4oh
Mkutano katika Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Getty Images/AFP/K. Betancur

Viongozi wa ulimwengu watapitisha azimio la kisiasa katika mkutano huu wa kwanza na wa aina yake tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili. Hali ya usalama imeimarishwa hasa kufuatia mlipuko wa bomu mwishoni mwa wiki uliowajeruhi watu 29 katika mji wa New York.

Watetezi wa haki za binadamu tayari wameshatoa lawama na kusema kuwa mkutano huu wa kilele haujapata ushirikiano wa kutosha wa kimataifa.

Shirika la Amnesty International limesema kuwa mkutano huu umepoteza nafasi ya kuwepo kwa mpango unaokidhi matakwa ya dunia nzima. Wakati huo huo shirika la Human Rights Watch limezitaja nchi kama Brazil, Japan na Korea ya Kusini kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo hazijishughulishi na swala la kuwahifadhi wakimbizi wakati ambapo baadhi ya nchi zimewachukuwa wakimbizi wachache tu ilihali zingine hazitaki kuwachukuwa wakimbizi kabisa.

Mkimbizi wa Afghanistan katika kambi Ugiriki
Mkimbizi wa Afghanistan katika kambi UgirikiPicha: Getty Images/M. Bicanski

Takriban wakimbizi milioni 65 wanahangaika kote duniani wakikimbia migogoro kama vile wa Syria. Watu hao wanakabiliwa na njaa na umasikini ikiwa ni pamoja na wakimbizi wengine milioni 21 wanaongonjea kupata fursa zilizo chache za kuhamishiwa katika nchi nyingine.

Wakimbizi wana matumaini viongozi watapata jawabu.

Mkutano huo wa kilele utaanza kwa hotuba za viongozi kutoka nchi mbali mbali katika baraza kuu la umoja wa mataifa huku hotuba zao zikitarajiwa kujikita zaidi katika mgogoro wa Syria.

Wakati wa mazungumzo ya kuelekea mkutano huo wa kilele pendekezo la katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon la kuwapa makaazi asilimia kumi ya idadi yote ya wakimbizi duniani liliondolewa kutoka kwenye rasimu ya azimio lisiloilazimisha nchi yoyote kulitekeleza.

Bibi Francoise Sivignon rais wa shirika la kutoa misaada la Medicins du Monde amesema smeeleza masikitiko yake kutokana na ukosefu wa mikakati ya kuwalinda wakimbizi watoto ambao wanakabiliwa na hali ngumu baada ya kutenganishwa kutoka kwa wazazi wao.

Rais Barack Obama wa Marekani ataongoza mkutano utaohudhuriwa na takriban nchi 40 katika kufanya maamuzi mapya ikiwa ni pamoja na kuwachukua wakimbizi zaidi au kutoa nafasi za elimu na ajira. Ni nchi nane tu hadi sasa ambazo zina wakimbizi ambao idadi yao ni sawa na nusu ya wakimbizi wote walioko duniani, nchi hizo ni Uturuki,Pakistan, Lebanon, Iran, Ethiopia Kenya na Uganda.

Nchi tajiri duniani za Marekani, China, Japan Ujerumani na Ufaransa zina jumla ya wakimbizi milioni 1.8 ikiwa ni asilimia 7 ya idadi ya wakimbizi wote duniani hayo ni kwa mujibu wa shirika la kutoa misaada la Oxfam kutoka Uingereza.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri:Yusuf Saumu