1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa amani Afghanistan kumalizika leo.

Halima Nyanza4 Juni 2010

Mkutano uliowakusanya viongozi wa kisiasa na makabila nchini Afghanistan, ambao una lengo la kutafuta njia za kumaliza vita vya miaka tisa sasa nchini humo, unamalizika leo mjini Kabul.

https://p.dw.com/p/NhjX
Wasdhiriki katika mkutano wa amani Jirga mjini Kabul, ambao unamalizika leo.Picha: AP
Takriban wajumbe 1,600, wanaowakilisha wanasiasa na viongozi wa kidini nchini Afghanistan wanahudhuria mkutano wa amani unaojulikana kama ''Jirga'' ulioanza siku ya Jumatano mjini Kabul, ambao wanasema kuwa mazungumzo na Wataliban ndio uamuzi mzuri na inawezekana kuwa nafasi ya mwisho ya kupatikana amani nchini humo. Kiongozi wa baraza la Ulemaa nchini Afghanitan na makamu mwenyekiti wa Jirga Qiamuddin Kashaf amesema iwapo watashindwa kufungua dirisha la amani kupitia mkutano huo wa jirga hawataweza kufungua njia ya amani kwa mustakabali wa nchi hiyo. Amesema wajumbe katika mkutano huo wameamua kuuufanya mkutano huo uwe na mafanikio kwani hilo ndilo tamko lao, kwamba hawataondoka katika mkutano huo wakiwa wameshindwa. Waratibu wa mkutano, wamesema wajumbe katika mkutano huo, waliitumia siku ya jana kwa kukaa katika makundi yapatayo 28, kujadili ni nani Rais Hamid Karzai wa nchi hiyo anapaswa kuwasiliana naye kwa mazungumzo ya amani na kwa vipi?. Tayari wajumbe wameanza kuwasilisha mapendekezo yao katika kikao cha leo kilichoanza mapema asubuhi, ambapo ndiyo siku ya mwisho ya mkutano huo. Wanadiplomasia wanasema kuwa makubaliano kama hayo ambayo yameungwa mkono kwa kiasi kikubwa yatamuongezea haki rais Karzai ya uongozi, wakati ambapo umaarufu wake kwa jamii ya Waafghan uko chini huku serikali yake ikizingatiwa kuwa isiyofaa na yenye rushwa. Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan de Mistura amesema mwaka huu ni mwaka wa Afghanistan kufanikisha malengo yake hayo ama kuyaharibu. Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton amesema nchi yake inataka kupata taarifa kamili kuhusiana na juhudi za Rais Karzai kuunganisha upya Taliban.

Mkutano huo mkubwa wenye lengo la kutatua tofauti na kuzungumzia matatizo yanayoikabili jamii hiyo ya Waafghanistan unaojulikana kama ''jigra'', ni sehemu muhimu katika ilani ya uchaguzi wa mwaka jana katika kampeni za rais Karzai kuchaguliwa tena, ingawa awali alisema kwamba hatazungumza na viongozi wa Taliban ambao wana mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda au wale ambao hawatataka kuacha mapigano. Washirika wa magharibi wa Rais Karzai, hususan Marekani na Jumuia ya Kujihami ya NATO wameelezea kuunga mkono mkutano huo kama tukio muhimu la kihistoria katika kukomaa kisiasa kwa Afghanistan baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Taliban mwaka 2001. Aidha Rais Karzai, ameahidi kuwapa nafasi za juu wapiganaji wa Taliban na pia kuwapa msamaha watakapokubali kumaliza vita. Hata hivyo kundi la Taliban limesema kwamba halitakubali majadiliano mpaka pale majeshi yote ya kigeni yatakapoondoka nchini humo. Mwandishi: Halima Nyanza(afp) Imepitiwa na:   Hamidou Oummilkheir