1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Arab League wataka kifo cha Arafat kichunguzwe

6 Septemba 2012

Mkutano huo kwa kauli moja umeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat kufuatia tetesi kwamba aliuwawa kwa kupewa sumu.

https://p.dw.com/p/164Jz
Mkutano wa mawaziri wa Umoja wa nchi za Kiarabu mjini Cairo
Mkutano wa mawaziri wa Umoja wa nchi za Kiarabu mjini CairoPicha: Reuters

Mawaziri waliokusanyika mjini Cairo katika makao makuu ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu hapo jana walitoa taarifa ya pamoja na kutaka paundwe tume huru ya Umoja wa Mataifa kuchunguza kifo cha Yassar Arafat.Tamko hilo limetolewa baada ya kufanyika mazungumzo yaliyohudhuriwa pia na rais Mahmoud Abbas wa Palestina.Siku ya Jumatano Mamlaka ya Wapalestina ilitoa ridhaa kwa ujumbe wa majaji wa Kifaransa kuingia Ukingo wa Magharibi kuchunguza tetesi kwamba Arafat alipewa sumu.

Itakumbukwa kwamba mwezi uliopita waendesha mashataka wa Ufaransa walianzisha uchunguzi kuhusu kifo cha kiongozi huyo wa zamani wa Wapalestina baada ya kituo cha televisheni cha Kiarabu cha Aljazeera kurusha kipindi maalum cha uchunguzi ambapo wataalamu wa Uswisi walibaini kwamba waligundua kiwango cha juu cha sumu aina ya Polonium ndani ya vitu vyake marehemu.Sumu hiyo kwa mujibu wa wataalamu hao ni aghalabu hutumiwa katika masuala ya kijeshi na kisayansi.

Aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat
Aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser ArafatPicha: AP

Ni sumu hii pia iliwahi kutumiwa kumuua aliyekuwa jasusi wa Kirusi aliyegeuka kuwa mkosoaji wa ikulu ya Kremlin Alexander Litvinenko mwaka 2006 mjini London baada ya kutiliwa ndani ya chai.Mkutano wa Cairo umeunga mkono hatua ya Palestina ya kutaka kuwa na hadhi ya mwanachama mwangalizi katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa.Aidha rais Mahmoud Abbas ameshasema kwamba mwezi huu atakwenda kuliomba baraza kuu la Umoja huo wa Mataifa kukubali ombi lao kufuatia kauli za mshikamano zilizotolewa kuanzia Doha kulikofanyika hivi karibuni mkutano wa nchi za Kiislamu na huko Iran katika mkutano wa nchi zisizoegemea upande wowote.

Palestina inaweza kupata hadhi hiyo endapo itafanikiwa kuungwa mkono na wingi mdogo wa kura za wanachama 193 wa baraza kuu la Umoja huo,kinyume na ilivyo katika baraza la usalama ambako Marekani na mshirika wake Israel zimekuwa zikiitumia kura ya turufu kuizuia Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja huo.

Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za Kirabu mjini Cairo pia walizungumzia wasiwasi wao juu ya vita vya Syria hasa kufuatia ripoti za kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadmu nchini humo.Kufuatia wasiwasi huo waziri mkiuu wa Qatari Hamad bin Jassem anayeongoza kamati ya mawaziri juu ya mzozo wa Syria alitwikwa jukumu na jumuiya hiyo kukutana na mjumbe wa kimataifa kuhusu mzozo huo Lakhdar Brahimi na kujadiliana njia mpya za kumaliza mateso wanayoyapata Wasyria.

Mkutzano wa Cairo
Mkutano wa CairoPicha: Reuters

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri :AbdulRahman Mohammed