1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa chakula Roma

17 Novemba 2009

Rais Mugabe astahiki kuwapo mkutanoni ?

https://p.dw.com/p/KZ08
Berlusconi (pekee) yuhoi ?Picha: AP

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo yamegusia mada mbali mbali kuanzia malalamiko ya wanafunzi wa vyuo vikuu humu nchini,mkutano wa hali ya hewa ulimwenguni ,ziara ya rais Obama nchini China,azma ya Chama cha FATAH kujitangazia uhuru na mkutano wa kilele mjini Roma juu ya ukosefu wa chakula duniani.

Gazeti la Leipziger Volkszetung alieandika:

"Kuwa Waziri mkuu wa Itali, Silvio Berlusconi, ndie kiongozi pekee wa dola kuu ya kiviwanda anaehudhuria mkutano huu wa kilele juu ya chakula, si busara kisiasa tu, bali ni ushahidi dhahiri-shahiri wa kiini-macho cha mikutano mikubwa kama hii .Mkutano huu umevunjwa hadhi yake kwa kuhudhuria kiongozi kama Robert Mugabe wa Zimbabwe ambae binafsi, ndie dhamana wa hali ya njaa nchini mwake.Mugabe hastahiki kuwa katika orodha ya wasemaji wa mkutano huu wa UM, bali jukwaa lake ni Mahkama kuu ya kimataifa...... "

Ama gazeti la Rhein-Zeitung linaandika kwamba, njaa duniani, inaweza tu kuondolewa ,ikiwa jukumu hili litawekwa mabegani mwa viongozi wa kisiasa na sio tu katika matangazo ya mwisho ya mikutano ya ulimwengu.Gazeti laongeza:

"Mataifa tajiri yanapaswa kuacha kuyakinga masoko yao na bidhaa kutoka nchi masikini.Na serikali za nchi masikini nazo , zinapaswa kujenga misingi itayoziwezesha kusaidiwa.Hii maana yake ,kupiga vita rushua na ufisadi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa kimkoa.Zipokee msaada wa dharura pale tu, kweli unapohitajika ....Ni katika hali hii tu , ndipo matunda mema ya juhudi za Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO ) yaweza kuvunwa."

China na Marekani, ni mapacha waliogandana kiuchumi.China, inaihitaji Marekani na Marekani, imekopa mno kwa China. Na hii, laandika gazeti la Westdeutsche Zeitung kuhusina na ziara ya sasa ya rais Obama nchini China ,yazilazimisha pande zote mbili kuwa washirika.Gazeti laongeza:

"Hatahivyo, licha ya hotuba wastani kabisa alioitoa rais Obama huko Shanghai, haiwezi kuwatia watu kitunga cha macho kutoona kuwa China na Marekani, sio tu washirika,bali katika maswali mbali mbali na maeneo mbali mbali ,ni washindani.Fikiria tu kinyanganyiro chao cha malighafi."

Gazeti la Süddeutsche Presse, linazungumzia azma ya mwanasiasa wa chama cha Palestina cha FATAH,Saeb Erekat , ya kujitangazia dola huru la wapalestina: gazeti linahisi:

"Mawazo kama hayo, hayatokani na ukweli wa hali ya mambo, bali zaidi , na hali ya kukata tamaa na kufadhahika.Kwani, wapalestina katika ardhi zilizokaliwa na Israel,hawendi mbele na wameishiwa na mbinu.Tangu miaka 18 iliopita, amani imekuwa ikizungumzwa tu mikutanoni,wakati katika ardhi zao huko Ukingo wa magharibi wa mto Jordan na Jeruselem ya mashariki ,ujenzi ukiendelea katika ardhi zao.Kila kukicha ,ardhi zaidi za waplestina, zinanyakuliwa kujenga maskani ya wayahudi,barabara na hicho kiitwacho "maeneo ya hifadhi za mazingira".Na dunia inatumbua macho tu."

Mwandishi: Ramadhan Ali /DPA

Uhariri: Abdul-Rahman