1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G-20 wafunguliwa London

Oumilkher Hamidou2 Aprili 2009

Walimwengu wamepania kuukosoa uchumi wa dunia

https://p.dw.com/p/HOnT
Viongozi wa mataifa 20 tajiri pamoja na malikia Elisabeth wa pili wa UengerezaPicha: AP

Katika wakati ambapo mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoendelea G-20 umefunguliwa rasmi hii leo mjini London,faharasa katika masoko ya hisa barani Asia na Ulaya zimepanda,zikisaidiwa na hali ya kupanda zaidi kuliko vile ilivyokua ikifikiriwa faharasa katika masoko ya hisa nchini Marekani hapo jana.

Mbali na mkutano huu wa kilele ,masoko ya hisa yanategemea pia mkutano wa benki kuu ya Ulaya unaotazamiwa kuteremsha hii leo kiwango cha riba na kufikia kiwango cha chini kabisa cha asili mia moja.

Katika masoko ya hisa macho yamekodolewa London unakofanyika mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia G-20, yanayowakilisha asili mia 80 ya utajiri wa dunia,mkutano unaotazamiwa kumalizika leo jioni.

Azma ya pamoja ya nchi hizo kutaka kuukwamua uchumi na kuimarisha sheria za fedha za kimataifa ndio mada kuu zinazojadiliwa katika wakati ambapo ulimwengu unatazamiwa kukabwa na kishindo kikubwa cha kupooza shughuli za kiuchumi ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1945,pakiwepo idadi kubwa ya watu wasiokua na ajira.

Katika wakati ambapo Marekani inapigania bajeti iongezwe ili kupambana na hali hiyo,Ujerumani na Ufaransa zinasita kuzidisha nakisi ya bajeti zao na badala yake zinadai ziimarishwe sheria za kimataifa dhidi ya nchi zinazowavutia wawekezaji wanaokwepa kulipa kodi za mapato pamoja pia na mashirika ya walanguzi.

Rais Nicolas Sarkozy anasema:

""Lakini tunasema hii ni fursa ya kihistoria ya kujenga ulimwengu wa aina mpya.Neno Historia limetamkwa na Angela Merkel.Na fursa hii hatutaki kuipoteza.Tuko katika karne nya 21,kwa hivyo ni wakati wa kujenga msingi wa sheria ya karne nya 21."

Rais Barack Obama ametuliza mdahalo jana aliposema nchi zinabeba jukumu la kuchukua hatua za pamoja na kujishughulisha na masuala ya pamoja badala ya mgawanyiko usiokua na maana."

Hata hivyo rais huyo wa Marekani amesisitiza nchi yake "haiwezi kuwa pekee injini ya ukuaji wa kiuchumi."

Nchi za G-20 zinatarajiwa pia kukubaliana kuzipatia madaraka makubwa zaidi taasisi za fedha za kimataifa mfano shirika la fedha la kimataifa IMf na kuahidi kutopitisha hatua za kujipendelea.

Pembezoni mwa mkutano huo,mji mkuu wa Uengereza London umegeuka uwanja wa machafuko ya makundi yanayopinga utandawazi-machafuko yaliyogharimu maisha ya mwanaharakati mmoja karibu na makao makuu ya benki kuu ya Uengereza.Chanzo halisi cha kufa kwake hakijulikani lakini.

Maandamano zaidi yanasubiriwa hii leo karibu na mahala mkutano huo wa kilele unakofanyika.

Muandishi;Hamidou Oummilkheir

Mhariri;Abdul Mtullya