Nchi tajiri zakubaliana kupunguza hewa chafu na kuendelea kushirikiana n...
9 Julai 2008Baada ya mkutano wao wa siku tatu nchini Japan viongozi wa nchi 8 tajiri wamekubaliana juu ya kupunguza hewa chafu, kuzisaidia nchi za Afrika, pamoja na kukabiliana na mifumuko ya bei za chakula na nishati.
Vingozi wa nchi hizo wamekubaliana kwa jumla juu ya kupunguza kwa nusu utoaji wa hewa chafu, Co2 hadi kufikia mwaka 2050.
Lakini viongozi hao hawakufafanua juu ya makubaliano yao ambayo hayakuungwa mkono na nchi zinazoinukia kiuchumi ,India na China.
Hatahivyo mkutano wa viongozi wa nchi za G8 umetathminiwa kuwa wa mafanikio na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hasa katika suala la kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kansela Merkel pia amesema viongozi wa nchi tajiri wamekubaliana juu ya kuimarisha ushrikiano na nchi zinazoinukia kama ilivyoazimiwa mwaka jana kwenye mkutano wa G8 uliofanyika Heiligendamm -Ujerumani. Bibi Merkel amesema wakuu wa nchi na serikali wa nchi tajiri wameazimia kutekeleza jukumu la kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
kuhusu Afrika nchi za G8 zimekubaliana kuendelea kuzisaidia nchi hizo kwa kutenga kiasi cha dola Bilioni 10 za haraka. Lakini mashirika ya misaada yamesema fedha hizo hazitasaidia kitu kutokana na mifumuko ya bei za chakula na nishati.
Kwenye mkutano wao viongozi wa nchi tajir pia walijadili suala la Zimbabwe. Viongozi hao wamependekeza kumpeleka mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Zimbabwe .
Nchi tajiri 8 duniani ambazo ni Marekani,Ujerumani,Ufaransa,Uingereza Japan,Canada ,Italia na Urusi zimekubaliana kutekeleza ahadi za hapo awali juu ya kuendelea kutoa kiasi cha dola bilioni 60 kwa ajili ya kupambana na maradhi. Viongozi wa nchi hizo wamesema watatekeleza ahadi walizotoa, katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hapo awali nchi hizo ziliahidi kutoa msaada wa dola bilioni 25 kila mwaka kwa ajili ya Afrika.