1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 kuanza Ijumaa

Grace Kabogo
5 Julai 2017

Mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa na yale yanayoinukia kiuchumi duniani, G20 unaanza Ijumaa na watajadiliana kuhusu vita, mabadiliko ya tabia nchi na biashara ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2fwyi
Logo G20-Gipfel

Masuala mengine yatakayotawala katika mkutano huo utakaofanyika mjini Hamburg, hapa Ujerumani ni pamoja na hatua ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya makombora hapo jana, usalama na mizozo ya kibiashara na kidiplomasia. Hata hivyo mkutano huo wa G20 ulitawaliwa na maandamano kutoka kwa wanaharakati wanaoupinga mkutano huo wa siku mbili.

Polisi wa Ujerumani walifanikiwa kuwatawanya waandamanaji hao wapatao 500 mjini Hamburg baada ya kutumia mabomu ya kutoa machozi. Msemaji wa polisi amesema baada ya mapambano ya usiku kucha, hali mjini Hamburg imerejea na kuwa ya utulivu na kwamba hakuna tena operesheni zaidi za polisi zinazoendelea.

Deutschland G20 Gipfel Proteste
Waandamanaji wa Hamburg wakipambana na polisiPicha: picture-alliance/dpa/C. Gateau

Zaidi ya waandamanaji 100,000 wanatarajiwa kujitokeza mjini Hamburg siku za mkutano huo, huku wakiwa na kaulimbiu inayosema ''Ushirikiano usio na mipaka, badala ya G20.'' Kiasi ya polisi 20,000 watakuwepo kwa ajili ya kuwalinda viongozi watakaohudhuria mkutano huo pamoja na kuwadhibiti waandamanaji hao.

Xi Jinping awasili Berlin

Tayari baadhi ya viongozi wameanza kuwasili kabla ya mkutano huo wa G20, ambapo Rais wa China Xi Jinping leo amewasili mjini Berlin ikiwa ni sehemu ya kufanya mazungumzo ya kidiplomasia. Xi alilakiwa kwa heshima ya kijeshi na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier kabla ya kuhudhuria mkutano wake na Kansela Angela Merkel.

Ratiba nyingine ya Xi ni kuitembelea bustani ya wanyama ya Berlin, ambapo yeye na mwenyeji wake Kansela Merkel watawaangalia Panda ambao waliwasili hivi karibuni Berlin ikiwa ni zawadi kutoka China. Jioni ya leo atahudhuria halfa iliyoandaliwa na Rais Steinmeier.

Deutschland China Xi bei Merkel
Rais Xi Jinping akiwa na Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/A. Schmidt

Xi na Merkel kwa pamoja watahudhuria mkutano wa kilele wa G20 siku ya Ijumaa na Jumamosi ambapo wanatarajiwa kuzungumzia ajenda kadhaa pamoja na viongozi wengine wa dunia ikiwemo sera za pamoja za mabadiliko ya tabia nchi na biashara ya dunia.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump leo anawasili Warsaw, Poland kwa ziara fupi na atakutana na viongozi wa Poland pamoja na Croatia. Pia Rais Trump atafanya mkutano wa pamoja na waandishi habari na kiongozi wa Poland, Andrzej Duda.

Trump anazuru Poland kabla ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa G20, ambapo pia atakutana na Rais wa Urusi, Vladmir Putin pamoja na viongozi wengine wa dunia.

US Präsident Trump
Rais Donald TrumpPicha: Picture alliance/AP Images/J. Locher

Wakati hayo yakijiri, mkutano mwingine umeanza leo mjini Hamburg, ikiwa ni kitendo cha hivi karibuni cha kuupinga mkutano wa kilele wa G20 utakaoanza baadae wiki hii.

Mkutano huo unaojulikana kama ''Mshikamano wa Kimataifa,'' utahusisha majadiliano yatakayoongozwa na majopo 12 na zaidi ya warsha 70 zinafanyika leo na kesho. Kwa mujibu wa tovuti iliyoandaa mkutano huo, masuala kadhaa yatajadiliwa ikiwemo umaskini, unyonyaji, unyayasaji, vita, uharibifu wa vitu vya asili pamoja na ubaguzi wa rangi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef