1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 waanza Japan

John Juma
28 Juni 2019

Miongoni mwa masuala tete yanayotarajiwa kuugubika mkutano huo wa kilele ni mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China, mvutano kati ya Iran na Marekani na mada kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3LELU
Japan G20 Gipfel Osaka
Picha: Reuters/K. Lamarque

Viongozi wa nchi 20 zenye nguvu zaidi ulimwenguni wanakutana nchini Japan. Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kuutawala mkutano huo wa kilele ni mvutano kati ya Marekani na Iran pamoja na mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China miongoni mwa mengine mengi.

Mkutano huo wa kilele wa siku mbili wa nchi 20 zenye nguvu zaidi duniani kiuchumi G-20, umeanza leo katika mji wa Osaka Japan.

 

Mkutano kati ya Trump na Xi

Miongoni mwa mikutano inayosubiriwa kwa hamu kubwa pembezoni mwa mkutano huo wa kilele, ni kati ya Rais Trump na rais wa China Xi Jinping kesho Jumamosi.

Nchi hizo mbili zimejikuta katika mvutano mbaya wa kibiashara na viongozi wengi wanasubiri kuona ikiwa viongozi hao wataweza kupata suluhisho la kumaliza uhasama.

Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe
Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Reuters/K. Mayama

Akizungumzia mkutano unaotarajiwa kesho kati yake na Xi, Rais Trump amesema hajamuahidi rais Xi kuwa hajatoa ahadi yoyote kwa Rais Xi kuacha kuongeza kodi za bidhaa lakini anatarajia mkutano wao kuwa wenye mafanikio.

"Tutaona yatakayojiri kwenye mkutano huo. Lakini tunaendelea vizuri, kama nchi Marekani ndilo taifa bora zaidi kwa sasa na uchumi uko sawa. Viongozi wote wamejitokeza na kupongeza yale ambayo yamefanyika Marekani.

Mvutano kati ya Iran na Marekani

Mzozo kati ya Marekani na Iran umeibua hofu ya uwezekano wa kusababisha vita ambavyo vinaweza kuathiri Mashariki ya kati. Na ni kati ya mada zinazotarajiwa kugubika mkutano huo.

Katika wiki za hivi karibuni, Marekani imeilaumu Iran kwa kushambulia meli sita za mafuta, madai ambayo Iran imekanusha. Wiki iliyopita Iran ilishambulia ndege inayopaa bila rubani ya Marekani ikisema ilipaa katika himaya yake.

Viongozi wa ulimwengu akiwemo kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamezihimiza nchi hizo kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya amani.

Kabla ya mkutano huo kufunguliwa, Rais Trump alikutana na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, kabla ya kufanya mazungumzo na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ataka maafikiano kuhusu namna ya kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ataka maafikiano kuhusu namna ya kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchiPicha: President Secretary/Laily Rachev

Rais Trump pia alikutana na rais wa Urusi Vladimir Putin na akamwambia huku akitabasamu tena kwa njia ya utani kuwa asiingilie kati uchaguzi wa Marekani.

Mabadiliko ya tabia nchi

Mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mada tete zinazotarajiwa kujadiliwa.

Ufaransa imesema inataka wanachama wa G20 wajitolee kuhakikisha viwango vya utoaji wa gesi chafu vinapungua na hilo liwe miongoni mwa maazimio ya pamoja ya mkutano huo.

Hata hivyo huenda Marekani isikubaliane na takwa hilo hasa ikizingatiwa, mwaka uliopita, Rais Trump aliiondoa nchi yake kwenye makubaliano ya Paris yam waka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Vyanzo: AFPE, DPAE,RTRE