1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7 waanza nchini Canada

Amina Mjahid
8 Juni 2018

Viongozi wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda G7 wanatarajiwa kutofautiana na rais wa Marekani Donald Trump wakati watakapomshinikiza kuondoa vikwazo katika bidhaa za chuma na bati.

https://p.dw.com/p/2zB1J
Japan Flaggen der G7-Mitgliedsstaaten 2016
Picha: picture-alliance/dpa/K. Ota

Kutofautiana huko kunatishia kuharibu sura ya kundi hilo la G7 ambapo kulingana na historia yake ya miaka 43 limejizatiti kupata suluhu ya kiuchumi na masuala mengine. Lakini Trump amesema anatarajia kutatua migogoro katika mkutano huo wa kilele.

"Natarajia kuondoa mipango dhaifu ya kibiashara na mataifa ya G7, isipofanyika, tutatoka tukiwa bora zaid!" alisema Trump kupitia ukurasa wake wa twitter, kabla ya kuondoka mjini Washington kuelekea mjini  Quebec, kunakofanyika mkutano huo.

Kanada Justin Trudeau und Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau Picha: Getty Images/AFP/I. Langsdon

Trump alitoa wito wa Urusi kurejeshwa katika kundi hilo la G7 baada ya kutolewa kufuatia kuingilia mgogoro wa Ukraine na kulitwaa eneo la Crimea mwaka 2014.

Akizungumza na waandishi habari hapo jana jioni afisa mmoja wa Canada alisema katika mkutano huo kutakuwepo na kutofautiana kwingi juu ya masuala tofauti.

Japokuwa Trump anasema kuwa ongezeko la ushuru kwa bidhaa za chuma na bati ni muhimu ili kulinda viwanda vya Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya wameitaja hatua hiyo kama isiyofaa na iliyo kinyume cha sheria na wanatayarisha mikakati ya kujibu.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemuonya Trump kwamba wanachama wengine wa G7 huenda wakaunda kundi lao iwapo itahitajika akisema hakuna kiongozi wa milele.  Lakini Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amewaambia waandishi habari kwamba angelitaka Umoja wa Ulaya ujizuwie katika majibu yake juu ya ushuru wa Marekani na kwamba majibu yanapaswa kuwa ya uwiano na unaofuata sheria.

Trump ataondoka mapema kabla ya kumalizika rasmi kwa mkutano wa G7 kuelekea Singapore kukutana na Kim Jong Un.

Hata hivyo Trump hakuonesha dalili yoyote ya kulegeza msimamo wake hii leo baada ya kuishutumu Canada na Ufaransa kwa kutoza ushuru wa juu zaidi kwa bidhaa za Marekani huku akimtuhumu Waziri Mkiuu wa Canada Justin Trudeau kuwa na jazba.

G7 Gipfel in Kanada Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Nchini Ujerumani maafisa wakuu wameitolea wito Ulaya kubakia kuwa kitu kimoja wakati wa wasiwasi wa kibiashara na Marekani huku wakisisitiza kuwa Marekani inabakia kuwa mshirika wake wa karibu nje  ya  bara hilo.

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya White House rais Trump anasemekana kuondoka siku ya Jumamosu kabla ya kumalizika rasmi kwa mkutano huo wa kilele wa G7 na kuelekea Singapore anakotarajiwa kukutana na rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Wakati viongozi wa G7 wakimpongeza Trump kwa juhudi zake za kuimarisha rasi ya Korea hawajafurahishwa na hatua yake ya kujiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran ulionuiwa kuizuwia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP

Mhariri: Gakuba, Daniel