1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa jumuiya ya kiarabu kuhusu amani ya Mashariki ya Kati waanza Libya

8 Oktoba 2010

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas ataelezea msimamo wake wa kusitisha mazungumzo ya ana kwa ana ya amani na Israel mpaka itakaporefusha marufuku ya ujenzi wa makaazi ya walowezi

https://p.dw.com/p/PZF0
Rais wa mamlaka ya Wapalestina, Mahmoud AbbasPicha: AP

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, leo (08.10.2010) atatoa taarifa kwa mawaziri 16 wa jumuiya ya kiarabu kuhusu mchakato wa amani, ambayo Julai 29 mwaka huu ilimruhusu kuanzisha tena mazungumzo ya ana kwa ana, baada ya kukamwa kwa miezi 20 kufuatia vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Nabil Abu Rudeina, msemaji wa rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, amesema kiongozi huyo ataziambia nchi za jumuiya ya kiarabu kwamba kurudi kwenye meza ya mazungumzo kunahitaji kwanza kusitishwa kabisa shugguli zote za ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi. Msemaji huyo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ujenzi wa makaazi ndicho kikwazo kikubwa kwa mazungumzo ya amani baina ya Israel na Wapalestina na unaweka mazingira ambapo Israel pekee ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa kuzuia mchakato huo wa kisiasa.

Rais Abbas amesema anataka kuendelea na mazungumzo lakini hawezi mpaka ujenzi wa makaazi mapya ya Wayahudi usitishwe kwa miezi mitatu au minne kuzipa nafasi juhudi za kutafuta amani. Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa upande wake anasema itakuwa huzuni kubwa kama rais Abbas, anayejulikana pia kama Abou Mazen, atajiondoa kwenye mazungumzo hayo kwa sababu ya suala ambalo halina msingi katika uwezekano wa matokeo ya mazungumzo hayo, ambao ni mkataba wa amani kuumaliza mzozo wa miaka 60 na kuunda taifa huru la Palestina.

Mwanadiplomasia mmoja wa Kiarabu amesema kutakuwa na kutupiana lawama na majukumu kati ya rais Abbas na jumuiya ya kiarabu, huku Abbas akitarajiwa kuitupia mpira jumuiya hiyo, akisema anataka kuungwa mkono. Jumuiya ya kiarabu inatarajiwa kutoa mwito wa pamoja kutaka mazungumzo ya amani yaungwe mkono, lakini viongozi wa jumuiya hiyo wataweka wazi kwamba uamuzi wa kuendelea na mazungumzo hayo uko mikononi mwa Abu Mazen.

Akizungumza siku moja kabla mkutano wa jumuiya ya kiarabu mjini Sirte, Libya, mpambe wa rais Abbas, Yasser Abed Rabbo, ambaye ni mmoja wa wapatanishi wa Palestina katika mazungumzo ya amani na Israel, amesema ni vigumu kuwa na mchakato wa maana wa amani na serikali ya sasa ya Israel inayoongozwa na waziri mkuu Netanyahu.

Mjini Sirte waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alimpigia simu rais Abbas kumwambia kuwa Marekani inaendeleza juhudi zake kuufanikisha mchakato wa amani. Wakati huo huo, balozi wa Israel nchini Marekani, Michael Oren, ameliambia gazeti la Washington Post hapo jana kwamba Marekani imeiahidi Israel vivutio vitakavyoiwezesha serikali kupitisha uamuzi wa kurefusha marufuku ya ujenzi wa makaazi ya walowezi, iliyomalizika Septemba 26 mwaka huu 2010.

Mkutano wa Sirte unafanyika kufuatia kuuwawa kwa Mpalestina mmoja mapema leo, baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel kwenye operesheni iliyofanywa katika mji wa kusini wa Hebron, huko Ukingo wa Magharibi.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman