1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Urusi

Oummilkheir18 Mei 2007

Hakuna makubwa yanayotarajiwa kufuaqtia mkutano huo wa kilele wa Samara

https://p.dw.com/p/CHE9
Kansela Angela Merkel na rais Putin
Kansela Angela Merkel na rais PutinPicha: AP

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na rais Vladimir Putin wa Urusi wanaendelea na mazungumzo yao “wa kuambiana ukweli “ hii leo katika wakati ambapo wapinzani mashuhuri ,akiwemo pia bingwa wa zamani wa dunia wa mchezo wa dama-Chess-Garry Kasparov wamezuwiliwa kujiunga na maandamano yanayofanyika karibu na mkutano huo wa kilele wa Samara.

“Tuko tayari kujadiliana kwa dhati na kwa uwazi kabisa-bila ya miko yoyote-ili kusaidia kumaliza mivutano iliyoko” amesema rais Vladimir Putin mnamo siku ya pili ya mkutano wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Urusi katika kituo cha mapumziko cha VOLJSKII OUTES-umbali wa kilomira 100 kutoka Samara-kusini-katika fukwe za Volga,kusini mwa Urusi.

“Tunabidi tufafanue wqazi kabisa,tunataka kuelekea wapi-tumekwama wapi na wapi tunaweza kwa pamoja kukabiliana na changa moto zinazojitokeza mfano ulinzi wa hali ya hewa na uchumi kuambatana na nishati”-ameshadidia kwa upande wake kansela Angela Merkel ambae nchi yake ndio mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya.

Kuondolewa vizuwizi vilivyowekwa na Urusi dhidi ya nyama ya Poland-uamuzi unaokorofisha duru mpya ya mazungumzo ya ushirikiano kati ya Umoja wa ulaya na Urusi,maguvu ya Urusi katika sekta ya nishati,mustakbal wa Kosovo,haki za binaadam na kujiunga Urusi na shirika la biashara la kimataifa ni miongoni mwa mada zinazopandisha mori kati ya umoja wa ulaya na Urusi.

Mwanzoni mwa kikao cha mashauriano hii leo,kansela Angela Merkel alisisitiza umuhimu wa “ushirikiano katika sekta ya nishati”.Umoja wa ulaya unataka kuanzisha utaratibu utakaodhamini kupatiwa mafuta katika wakati ambapo mivutano kati ya Moscow na majirani zake imeshapelekea kusitishwa kwa ghafla shughuli za kusafirishwa gesi au mafuta ghafi ya Urusi kuelekea nchi za Ulaya.

Katika karamu ya chakula cha usiku jana,kansela Angela Merkel alisisitiza juu ya umuhuimu wa “kutatuliwa mzozo wa nyama ya Poland na kuanza haraka kujadiliana kuhusu “aina mpya ya ushirikiano kati ya umoja wa ulaya na Urusi.

Ushirikiano kama huo unaangaliwa kua ni muhimu kwa Umoja wa ulaya unaoagizia robo ya mafuta yake kutoka Urusi –umoja ambao unasalia kua mshirika mkubwa wa kiuchumi wa Urusi.

Mwenyekiti wa Umoja wa ulaya,kansela Angela Merkel amesema:

“Ni vyema na muhimu kuhakikisha kwamba mikutano ya kilele inaendelezwa kila kwa mara kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi.Mkutano huu wa sasa unafanyika pakiwepo hali ya mivutano sawa na masuala ya pamoja yanayobidi kuzingatiwa.Lakini umuhimu mkubwa zaidi ni ile hali kwamba tunazungumza kwa uwazi kabisa juu ya kila suala na kuendelea kubadilishana fikra.”

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya José Manuel Barroso ameshadidia kwa upande wake umuhimu wa “Demokrasia na haki za binaadam-mada inayowakera viongozi wa Urusi na kuuteremshia kiwingu mkutano huu wa kilele.

Wakati huo huo wanaharakati kadhaa wa upande wa upinzani,akiwemo bingwa wa zamani wa dunia wa mchezo wa Dama-Chess ,Garry Kasparow, walizuwiliwa wasiondoke Moscow kwenda Samara kushiriki katika maandamano dhidi ya rais Putin.

“Wametuzuwia,tulikua watu 25 pamoja na Kasparov tusipande ndege”-amesema kwa simu mkuu wa chama cha kibolsheviki Edouard Limonov.

Upande wa upinzani umepanga kuitisha maandamano leo jioni kulalamika dhidi ya siasa ya rais Vladimir Putin.