1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Charm el Sheikh

Oummilkheir21 Juni 2007

Mahmoud Abbas ategemea kupata uungaji mkono wa Israel,Misri na Jordan watakapokutana Misri jumatatu ijayo

https://p.dw.com/p/CB3Q
Mahmoudn Abbas na waziri mkuu wa serikali ya dharura Salam Fayyad
Mahmoudn Abbas na waziri mkuu wa serikali ya dharura Salam FayyadPicha: AP

Rais Mahmoud Abbas wa Palastina,aliyedhoofika baada ya ushindi wa Hamas huko Gaza,anategemea uungaji mkono wa Misri,Jordan na Israel,mkutano wa kilele kati ya nchi za kiarabu na Israel utakapoitishwa nchini Misri jumatatu ijayo.

Mkutano wa kilele wa pande nne utakaowaleta pamoja Mahmoud Abbas,waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert,mfalme Abdallah wa pili wa Jordan na rais Hosni Mubarak wa Misri utafanyika katika mji wa mwambao wa Charm el Sheikh katika bahari ya Sham.Msemaji wa rais wa utawala wa ndani wa Palastina,Nabil Abou Roudeina amesema tunanukuu:”Mkutano huo wa kilele wa pande nne utaitishwa jumatatu ijayo kutokana na mwaliko wa rais Hosni Mubarak “Mwisho wa kumnukuu msemaji wa rais wa Palastina.

Israel,Misri na Jordan zimethibitisha mkutano huo utafanyika-wa kwanza wa aina yake tangu mkutano kama huo kuitishwa February nane mwaka 2005 huko huko Charm el Sheikh,akihudhuria lakini wakati ule waziri mkuu wa zamani wa Israel Ariel Sharon na viongozi hao hao watatu wa kiarabu.

“Mkutano wa kilele umelengwa kuupa msukumo uhusiano kati ya utawala wa ndani wa Palastina na Israel-amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Abou Gheit aliyeongeza kusema tunanukuu “Umelengwa pia kuufufua utaratibu wa amani ya mashariki ya kati.”

Msemaji wa waziri mkuu wa Israel amekiri kwamba mkutano wa kilele wa Sharm el Sheikh umelengwa kuwapa moyo wafuasi wa siasa za wastani na kupalilia uhusiano kati ya Israel na Palastina.

Kwa mujibu wa Miri Eisin,waziri mkuu Ehud Olmert amekua akizungumza kwa simu kila kwa mara pamoja na rais Hosni Mubaraka wa Misri na mfalme Abdallah wa pili wa Jordan.

Akiulizwa kwa jinsi gani Ehud Olmert anaweza kumsaidia Mahmoud Abbas,msemaji huyo wa waziri mkuu wa Israel Miri Eisin amesema Ehud Olmert anapanga kuliomba baraza la mawaziri jumapili ijayo liruhusu upya kupatiwa wapalastina fedha zao zilizozuwiliwa na Israel.

Waziri mkuu Ehud Olmert aliyeonana na rais Bush wa Marekani jumanne iliyopita,ameelezea azma ya kutaka kuzungumza kwa dhati na Mahmoud Abbas juu ya uwezekano wa kuundwa dola la Palastina.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel Tzipi Livni amezungumza kwa simu jana pamoja na waziri mkuu wa serikali ya dharura ya Palastina Salam Fayyad anaeungwa mkono na jumuia ya kimataifa.

Hamas wanaolidhibiti eneo la Gaza kufuatia mapigano ya wiki moja yaliyogharimu maisha ya watu 115 hawataki kuitambua serikali hiyo.

Mjini Ramallah,taasisi muhimu ya chama cha ukombozi wa Palastina imetoa mwito wa kuitishwa uchaguzi mkuu wa kabla ya wakati ,bila ya kuwashirikisha Hamas.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma,asili mia 75 ya wapalastina wanaunga mkono fikra hiyo na wanaamini Mahmoud Abbas na chama chake cha Fatah wataibuka na ushindi hata kama Hamas watashiriki.