1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa COMESA waanza

26 Februari 2014

Mkutano wa kilele wa 17 wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) umefunguliwa, huku mwenyekiti anayemaliza wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda akisisitiza amani na biashara huru.

https://p.dw.com/p/1BFTZ
Mwenyekiti wa COMESA anayemaliza muda wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Mwenyekiti wa COMESA anayemaliza muda wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: picture alliance/empics

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi iliyochukuwa takribani dakika 20 katika ofisi za Umoja wa Afrika, mjini Kinshasa , Rais Museveni amesema "hakutokueko na maendeleo bila amani ya kudumu" na kwa hivyo amehimiza marais wenzake kuhakikisha panakuwapo juhudi za pamoja katika kuboresha miradi ya maendeleo.

Wakati wa kuwasili kwake mjini Kinshasa, Rais Museveni aliiambia DW kwamba matarajio makubwa ya raia wanaoishi kwenye eneo la COMESA ni amani.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye amewakilisha nchi yake kwenye mkutano huo, amesema kwamba matarajio makubwa ya mkutano wa Kinshasa ni kuunda ajira kwa vijana.

Mada kuu ya mkutano huu wa siku mbili ni maendeleo ya kudumu kupitia katika kuunda viwanda vidogovodogo na vya kadiri. Marais saba wanahudhuria mkutanao huu, akiwemo Rais Museveni, Michael Sata wa Zambia, Joyce Banda wa Malawi, Omar al-Bashir wa Sudan, Robert Mugabe wa Zimbabwe, Ismael Omar Guelleh wa Djibouti na mwenyeji wao, Joseph Kabila wa Kongo.

Rwanda na Burundi zimewakilishwa na waziri mkuu na makamu wa pili wa rais, huku nchi nyingine 10 wanachama zikiwa zimewakilishwa kwa ngazi ya mawaziri.

Mkutano huo wa kilele ulifunguliwa kwenye ukumbi wa Union Africaine mjini Kinshasa.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef