1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa G-20 wamalizika mjini London

Oumilkher Hamidou2 Aprili 2009

Shirika la fedha la kimataifa na shirika jengine la fedha yamepewa jukumu la kubuni sheria mpya za masoko ya fedha

https://p.dw.com/p/HP3a
Viongozi wa G 20 wamzunguka rais wa China Hu JintaoPicha: AP

Viongozi wa kundi la mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia-G-20 wanaokurubia kumaliza mkutano wao mjini London wanasemekana wamekubaliana kubuni sheria mpya za shughuli za fedha na kuzidisha mara tatu hazina ya shirika la fedha la kimataifa IMF. "Masoko ya hisa yanaendelea vyema huku faharasa zikipanda tangu Ulaya,Asia na pia Marekani.


Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho ambayo nakala yake imelifikia shirika la habari la Reuters,viongozi wa mataifa 20 tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia duniani wameahidi kusimamia mashirika ya walanguzi na kubuni sheria itakayosimamiwa na taasisi maalum pamoja na shirika la fedha la kimataifa yatakayokua na madaraka ya kutosha.


Kwa mujibu wa duru za taasisi za fedha na duru za wajumbe wa kutoka nchi zinazoinukia,taarifa ya mwisho inazungumzia juu ya kutolewa kitita cha dala bilioni 500 za ziada kuongezea hazina ya shirika la fedha la kimataifa itakayofikia dala bilioni 750.Shirika hilo la fedha litaruhusiwa pia kukopa katika masoko ya hisa.


""Maendeleo makubwa yamepatikana kwa namna ambayo watu wanaweza kuamini kwamba taasisi za kimataifa mfano wa IMF yana fedha zinazohitajika kuweza kutekeleza shughuli zake ipasavyo na haraka zaidi kuliko zamani" amesema hayo waziri wa fedha wa Uengereza Alistair Darling alipokua akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Tv.


Japan na Umoja wa Ulaya wameshasema watatenga dala bilioni 100 na Marekani imeahidi pia kutenga dala bilioni mia moja.


Viongozi wa G20 wanasemekana wanakurubia kufikia makubaliano kuhusu mpango wa kuunga mkono shughuli za kibiashara ulimwenguni-kwa kitita cha dala bilioni 250.Waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown alipendelea kitita hicho kisiwe chini ya dala bilioni 100.



Mkutano wa kilele wa G-20 waonyesha kuzusha matumaini mema kwa masoko ya hisa ya kimataifa.Mjini New-York,faharasa katika soko la hisa la Wall Street zimezidi kupanda.


Hatua kali za ulinzi zimeimarishwa mahala ambako mkutano huo wa kilele umekua ukifanyika.Vikosi vya polisi vinapiga doria katika wakati ambapo wanaharakati wanaopinga utandawazi wamepania kuandamana tena hii leo.


Huu ni mkutano wa pili wa kilele wa G-20 baada ya ule uliotishwa mjini Washington November mwaka jana.

Muandishi: Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman