1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa G 20

Hamidou, Oumilkher14 Novemba 2008

Viongozi wa mataifa tajiri kiviwanda na wenzao wa mataifa yanayoinukia wakutana Washington

https://p.dw.com/p/Furz
Rais George W. Bush akihutubia kuhusu mzozo wa fedha mjini WashingtonPicha: AP



Mataifa tajiri kabisa kiviwanda na mataifa yanayoinukia-G20 yanakutana kwa dharura hii leo  mjini Washington kujaribu kuituliza zahma mbaya kabisa ya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1929,katika wakati ambapo vitisho vya kudorora uchumi wa dunia vinazidi kubainika.



Kwa muda wa siku mbili,washiriki mkutanoni watajitahidi kuupatia ufumbuzi mzozo uliopo na kusaka njia za kuzuwia mzozo kama huo usiripuke tena siku za mbele.


Kwa mara ya kwanza katika historia yake,uchumi wa nchi za zoni ya yuro umeanza kuzorota.Dola kuu la kiuchumi,Ujerumani pamoja na Italy ambayo ni  ya tatu miongoni mwa kundi la nchi 15 zinazotumia sarafu ya Yuro,zimetangaza rasmi kwamba shughuli zao za kiuchumi zimekwama.


Marekani ambayo hapo awali ilikua ikisita sita,hivi sasa imesema inapendelea mkutano wa kilele wa G-20 uidhinishe "mpango wa kimkakati" kuufanyia marekebisho mfumo wa fedha wa kimataifa.


Hata hivyo Marekani inapinga kuwepo taasisi ya kimataifa kushughulikia shughuli za fedha na haitaki pia kubebeshwa pekee jukumu la mzozo huu wa fedha.


"Mzozo huu  si matokeo ya kushindwa uchumi wa soko huru.Na jibu sio kuubadilisha mfumo wa soko huru amesema rais George W. Bush katika hotuba yake kuhusu hali ya kiuchumi na kuendelea kusema:


"Ukitaka ukuaji wa kiuchumi,ukitafuta fursa,ukitaka haki ya kijamii ,muruwa na utu,basi mfumo wa soko huru ndio njia ya kufuatwa.Litakua kosa kubwa kuruhusu miezi michache ya mzozo kuvuruga ufanisi wa miaka 60."


Rais George W. Bush hana nafasi kubwa ya kuutetea kwa ufanisi msimamo wake huo,seuze tena amesaliwa na miezi miwili tuu hadi mhula wake utakapokamilika na Barack Obama kuapishwa kama rais mpya wa Marekani january 20 mwakani.


Kwa upande wao viongozi wa Ulaya wanakiri pia kwamba mkutano wa kilele wa Washington hautapelekea kuchipuka Bretton Woods" ya pili,ikimaanisha makubaliano ya mwaka 1944 yaliyopelekea kubuniwa mfumo huu wa sasa wa fedha .


Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,Jose Manuel Barroso ameonya hii leo "watu wasitegemee  miujiza wakati wa mkutano huo wa kilele-"Huu ni mwanzo tuu" amesisitiza bwana Barroso.


Ameelezea hata hivyo matumaini yake kuona maamuzi thabiti yanapitishwa akikumbusha Umoja wa ulaya unapendelea kuona shirika la fedha la kimataifa linawajibika zaidi.


Kansela Anegla Merkel ameashiria "majadiliano magumu" akisisitiza juu ya umuhimu wa kutiwa njiani kwa kila hali mageuzi katika kipindi cha miezi ijayo.