1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa waanza

24 Septemba 2014

Viongozi kutoka zaidi ya nchi 140 wamefungua mkutano wao wa kila mwaka katika Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, ambapo wanakabiliwa na migogoro chungu nzima ambayo huenda haina ufumbuzi kamili

https://p.dw.com/p/1DJpY
UN Klimakonferenz 2014 in New York 24.09.2014 - Ban Ki-moon
Picha: Reuters/M. Segar

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo wa kila mwaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito kwa viongozi wa ulimwengu kutafuta kile alichokiita kuwa ni “mbegu za matumaini” katika hofu na kukosa matumaini ya ulimwengu unaoonekana kusambaratika.

Ban ameitaja migogoro inayoendelea kurundika ulimwenguni, magonjwa yanayosambaa, kurejea kwa mizimu ya enzi za Vita Baridi, na pia athari zinazotokana na vuguvugu wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu.

Suala ambalo bila shaka linatarajiwa kupewa kipaumbele miongoni mwa mada kuu katika kikao hicho ni kitisho kutoka kwa magaidi wenye itikadi kali za kiislamu cha kuinyakua mipaka. Wanadiplomasia wengi wanatumai kuwa mzozo huo hautaficha shida wanazopitia mamilioni ya raia wanaojikuta katikati ya migogoro hii nchini Syria, Iraq, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan kusini, Ukraine na Ukanda wa Gaza, masaibu ya idadi kubwa zaidi ya wakimbizi tangu kumalizika kwa Vita vya Pili Vikuu vya Dunia, na uungwaji mkono wa kimataifa kwa malengo mapya ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na umaskini na kuangazia suala la mabadiliko ya tabia nchi.

UN Klimakonferenz 2014 in New York 24.09.2014 - Barack Obama
Rais wa Marekani Obama amezungumzia masuala kadhaa yanayoukumba ulimwengu kwa wakati huuPicha: picture-alliance/dpa/Andrew Gombert

Kwenye hotuba yake katika mkutano huo, Rais wa Marekani Barack Obama amezungumzia zaidi kitisho cha ugaidi ulimwenguni. Obama pia ataongoza mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baadaye leo ambapo wanachama wanatarajiwa kuidhinisha azimio ambalo litalihitaji nchi zote kuzuia usajili wa usafirishaji wa wapiganaji wa kigeni wanaojiandaa kujiunga na makundi ya kigaidi kama vile Dola la Kiislamu.

Ufunguzi wa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, ambao unakamilika Septemba 30, unafuatia mkutano wa ngazi ya juu kabisa kuwahi kuandaliwa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, ambapo karibu viongozi 120 wa ulimwengu waliujadili wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuongeza kasi ya kisiasa katika kulitatua suala la ongezeko la joto duniani.

Viongozi wawili maarufu ambao hawajafika mjini New York kwa mkutano huo ni Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf kwa sababu ya mgogoro wa Ebola ambao umeiathiri taifa lake kwa kiasi kikubwa na Rais wa Ukraine Petro Poroshenko, ambaye hakutangaza sababu ya kutoshiriki kwake.

Mwandishi: BRUCE Amani/AP
Mhariri: Mohammed Khelef