1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kupambana na unyanyasaji wa kingono waanza Vatican

Amina Mjahid
21 Februari 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki papa Francis ameufungua mkutano wa kilele mjini Vatican wa kupambana na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto akisema dunia inatarajia hatua madhubuti kupiga vita unyanyasaji huo kanisani.

https://p.dw.com/p/3DmND
Vatikan Papst Franziskus bei der Eröffnung des Mißbrauchsgipfels in Vatikan
Picha: Getty Images/AFP/V. Pinto

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema watu watakatifu wa mungu wanatizama na kusubiri sio tu kukosolewa kwa unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, lakini wanasubiri kuona hatua na mikakati dhabiti ikichukuliwa dhidi ya suala hilo.

Akizungumza katika hotuba yake alipokuwa anaufungua mkutano huo ulioanza leo na kutarajiwa kumalizika siku ya Jumapili, Papa amewataka maaskofu kuja na majibu yanayofaa na thabiti ya kupambana na unyanyasaji huo wa kingono dhidi ya watoto.

Vatikan Gipfel zum Thema sexueller Missbrauch in der Kirche
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis akiongoza mkutano wa kilele juu ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watotoPicha: Getty Images/V. Pinto

Papa Francis pia amemuomba mama Maria kuwaongoza maaskofu wanaohudhuria mkutano huo katika jaribio lao la kuponya makovu ya kashfa za unyanyasaji wa kingono kwa watoto na kwa waumini huku akisema ni lazima wasikilize kilio cha watoto wanaodai haki zao.

Mkutano huo wa siku nne umeanza leo asubuhi kwa maombi na utajumuisha hotuba, mafunzo na warsha juu ya kuwalinda watoto, kuzuwia unayasaji na kuficha madhambi hayo. Hata hivyo wahanga wa unyanyasaji wametoa wito wa uwazi, kutovumiliana katika visa hivi viovu na uwajibikaji wa viongozi wakuu wa kidini wanaowaficha au kuwatetea wabakaji.

Kanisa katoliki laombwa kutoa majina ya watuhumiwa wa unyanyasaji wa kingono

Hapo jana wahanga hao walitaka kukutana na Papa Francis  mwenyewe lakini  baadaye walikutana kwa saa mbili na wanachama wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa kilele   juu ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

Kukusanyika kwa viongozi 190 wa kanisa katoliki mjini Vatikan kunafanyika wakati kukiwa na uchunguzi wa rekodi ya kanisa katoliki baada ya madai mapya ya unyanyasaji na kuficha yaliofanyika mwaka uliopita yaliyozua kutoaminika kwa viongozi wa kanisa hilo.

Vatikan Gipfel zum Thema Missbrauch in der Kirche
Baadhi ya maaskofu wa kikatoliki mjini VaticanPicha: Reuters/R. Casilli

Zaidi ya miaka 30 wakati kisa cha kwanza cha nyanyasaji wa kingono kilipoibuka katika kisiwa cha Ireland na nchini Australia na miaka 20 baada ya hali kama hiyo kutokea nchini Marekani maaskofu na viongozi wengine wakuu wa kanisa katoliki katika maeneo mengi ya Ulaya na Amerika ya Kusini na Asia ama wamekataa uwepo wa visa kama hivi au kutolichukulia kwa uzito tatizo hili.

Phil Saviano, aliesaidia kufichua kashfa ya unyanyasaji nchini Marekani miongo miwili iliopita ametaka kanisa hilo kutoa majina ya watuhumiwa wa unyanyasaji wa kingono pamoja na mafaili yao yalio na data zao muhimu. Saviano amesema hilo likifanyika basi litavunja ukimya uliopo wa kanisa katoliki juu ya visa vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, kuonyesha heshima kwa wahanga wa unyanyasaji na hata kuzuwiya vitendo zaidi kutokea.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/AP

Mhariri: Yusuf Saumu