1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa SADC.

Halima Nyanza16 Agosti 2010

Viongozi wa mataifa kutoka katika jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC wameanza rasmi mkutano wa siku mbili hii leo, katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek.

https://p.dw.com/p/OoZU
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe (kushoto) akiwa na Waziri mkuu wa nchi hiyo Morgan Tsvangirai, ambao serikali yao ya Umoja wa kitaifa inajadiliwa leo katika mkutano wa kilele wa SADC mjini Windhoek.Picha: picture alliance/dpa

Ajenda ya kikao hicho ni kuyajadili masuala ya ushirikiano katika kanda hiyo na hatua zilizopigwa za maendeleo ya kisiasa nchini Zimbabwe.

Mkutano huo wa kilele, unafanyika huku kukiwa na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo yenye wanachama 15, lakini sherehe hizo  zikikumbwa na hali ya kukosolewa juu ya jumuiya hiyo ya SADC kushindwa kutoa sura ya kuwa ni nguvu  ya kisiasa ya kutegemewa katika ukanda huo.

Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini ambaye anasaidia juhudi za upatanishi zinazofanywa na jumuia hiyo nchini Zimbabwe, atawaarifu viongozi hao wa nchi za SADC hatua iliyopigwa katika serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa kati ya Rais Robert Mugabe na kiongozi wa zamani wa upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai.

Süsafrika Jacob Zuma nach der Wahl
Rais Jacob Zuma.Picha: AP

Rais Zuma aliitembelea Zimbabwe mwezi Machi mwaka huu, kuwashinikiza viongozi hao wanaopingana, kusonga mbele na marekebisho na kumaliza tofauti zao juu ya uteuzi wa nafasi muhimu za uongozi serikalini.

Kulingana na mkataba huo wa kushirikiana madaraka, Zimbabwe ilipaswa mwezi uliopita kuendesha kura ya maoni kuhusiana na katiba mpya, ambayo ingefungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi mpya baada ya ghasia zilizotokea katika uchaguzi wa 2008.

Madagascar pia kujadiliwa:

Katika mkutano huo wa kilele, mzozo wa kisiasa nchini Madagascar pia utajadiliwa, kutokana na hali kutokuwa shwari tangu mwezi Machi mwaka uliopita, baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Marc Ravalomanana kupinduliwa na Andry Rajoelina.

'
Madagaskar Unruhen Andry Rajoelina Bürgermeister von Antananarivo
Andry Rajoelina.Picha: AP

Juhudi za SADC kusuluhisha mzozo huo zimekuwa na mafanikio kidogo, huku Rajoelina akikataa masharti yaliomo katika makubaliano ya kugawana madaraka.

Wiki iliyopita Rajoelina alitia saini makubaliano na vyama 99 vya kisiasa, ikiwemo kinachoongozwa na Marc Ravalomanana, makubaliano ambayo yanataka kura ya maoni juu ya katiba ifanyike mwezi  Novemba, uchaguzi wa bunge mwezi Machi na awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Rais Mei nne, mwaka ujao, wa 2011.

Jumuiya ya SADC imeisimamisha uanachama Madagascar mpaka pale itakapoheshimu katiba.

Kabila atakiwa kuunda tume huru ya uchunguzi:

Katika hatua nyingine wakati mkutano huo wa kilele wa SADC, ukifanyika leo, mashirika ya haki za binadamu yamemtaka mweyekiti wa SADC, anayemaliza muda wake Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuanzisha tume huru ya uchunguzi, kuhusiana na kifo cha mwanaharakati wa haki za binadamu nchini humo Floribert Chebeya aliyeuawa mwezi June mwaka huu.

Joseph Kabila
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: AP Photo

Katika barua ya wazi waliyomuandikia Rais Kabila, mashirika yapatayo 70 yanataka ufanyike uchunguzi, juu ya mauaji hayo na juu ya kupotea kwa dereva  wa mwanaharakati huyo aliyeuwawa.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Abdul-Rahman