1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Shirka la Kazi Duniani, ILO, umemalizika

Miraji Othman17 Juni 2009

Maneno matamu , lakini maamuzi machache katika mkutano wa kilele wa ILO.

https://p.dw.com/p/INYA
Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, akihutubia kikao cha 98 cha Shirika la Kazi Duniani, ILO, mjini Geneva, Uswissi.Picha: AP


Watu zaidi na zaidi wanafanya kazi bila ya kuwa na mikataba ya kazi, na bila ya kuwa na bima za huduma za kijamii. Na zaidi na zaidi kuna watu wasiokuwa na tamaa ya kupata ajira. Katika mkutano wa kilele wa siku tatu, Shirika la Kazi Duniani, ILO, lilitaka kuyazungumzia matatizo hayo yanayozidi, na pia suala la kupambana na umaskini unaotokana na hali hiyo. Lakini nchi 183 wanachama wa ILO hazijawa na hamu kubwa ya kuyasikiliza hayo.

Shirika la Kazi Duniani, ILO, ambalo lina makaazi yake huko Geneva, linatarajia kwamba, kutokana na mzozo wa kiuchumi na kifedha duniani, kutaengezeka sana idadi ya watu wasiokuwa na kazi duniani. Pia hali za kufanya kazi zitazidi kuwa mbaya. Hivyo, shirika hilo limetaka kuowanishwa hatua za kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo, makisio na matakwa hayo hayajatiliwa maanani vya kutosha na nchi wanachama wa Shirika la ILO. Kwani katika mkutano wa kilele wa dunia juu ajira huko Geneva, walikwenda wakuu wa nchi na serekali kutoka mataifa 15 au manaibu wao. Na kati ya hao, hasa rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, alilitumia jukwaa hilo kuubeza mfumo wa fedha wa kibepari ambao hauna mwelekeo, utanda wazi usiokuwa na kanuni ambapo sheria ya mwituni ndio inayotawala. Nicolas Sarkozy alilalamika juu ya mantiki ya ushindani wa kibiashara, ambapo wasiojiweza wanakwekwa kando, mazingira yanachafuliwa na mifumo ya fedha inaharibiwa. Alitaka utanda wazi lazima utilie maanani kuendeleza huduma za afya, elimu na utamaduni pamoja na kuunda nafasi za kazi, vitu ambavyo si bidhaa au mali ghafi.

Haya yote ni maneno mazuri kutoka mdomo wa rais wa Ufaransa, lakini hajatoa kabisa hata pendekezo moja thabiti juu ya siasa mbadala, na namna ya kupambana na ukosefu wa nafasi za kazi duniani. Na hasa kwa Ufaransa, nchi ambayo ndani ya Umoja wa Ulaya inaendeleza siasa ya kibiashara na ya kiuchumi inayojipendelea yenyewe tu bila ya kuwajali wengine. Kwa miaka nchi hiyo imekuwa ikizuwia kuondoshwa ruzuku kwa bidhaa za kilimo za nchi za Jumuiya ya Ulaya, jambo ambalo limewaathiri sana wakulima wadogo wadogo wa nchi za Afrika. Ukweli huo uliashiriwa pembezoni mwa mkutano huo wa kilele na baadhi ya jumuiya zisizokuwa za kiserekali pamoja na viongozi wa vyama vya wafanya kazi.

Mwishowe pia kulilaumiwa kwa haki kabisa kwamba serekali za nchi nyingi, hata kabla ya mzozo huu wa sasa wa kifedha na kiuchumi duniani, hazijatekeleza kabisa au si kwa kiwango cha kutosha yale masharti ya kazi yaliotokana na ahadi nchi hizo zilitzotoa katika mkataba wa Shirika la ILO.

Hata hivyo, kwa ujumla, majadiliano ya mkutano huo wa kilele wa ILO hayajaufanyia haki kabisa ukubwa na sura ya mzozo wa sasa wa kiuchumi duniani. Jee mipango ya kuupiga jeki uchumi, kupitia uzalishaji wenye nguvu wa bidhaa na pia biashara, kwa lengo la uchumi kukuwa, jee hiyo bado ndio njia ilio sawa ya kuunda nafasi zaidi za ajira? Jee mbinu hiyo ya kukuwa uchumi, ambayo hadi sasa imepelekea nishati zaidi itumike na mazingira yachafuke, kweli inawezekana na kukubalika, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani na kupunguka mafuta ya petroli? Kwamba masuala haya ya kimsingi hayajazungumziwa katika mkutano wa kilele wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, ni kuzubaa kukubwa kabisa.


Mwandishi:Andreas Zumach/ZR/Othman Miraji

Mhariri:Abdul-Rahman