1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika kufanyika wiki ijayo

Sekione Kitojo
18 Januari 2018

Viongozi  wa  mataifa  na  serikali  katika  bara  la  Afrika watakusanyika  kwa  ajili  ya  mkutano  wao  wa  kilele  mjini  Addis Ababa  Januari 22, mwaka  huu. Masuala  mawili  magumu yatakuwa mbele  yao  kuyajadili.

https://p.dw.com/p/2r6dz
Unterzeichnung Friedensabkommen im Kongo
Picha: Reuters

Masuala  hayo  ni  pamoja  na  Mageuzi  na  fedha. Wachambuzi  wanatarajia majadiliano  makali   katika  mkutano  huo. 

Iwapo  maneno  ndio  msingi  wa  kila  kitu,  basi  Afrika  imara  na yenye  amani  ni  kipaumbele  kikubwa  kwa  viongozi  wengi  wa  Afrika. Lakini  suala  kuu  kwa  viongozi  hao  watakaohudhuria  mkutano  wa kilele  wa  30  wa  Umoja  wa  Afrika watatafuta  mikakati  juu  ya  vipi hali  hiyo  inaweza  kupatikana. mkutano  huo  muhimu  utaanza  rasmi katika  makao  makuu  wa  Umoja  huo  katika  mji  mkuu  wa  Ethiopia, Addis Ababa Januari  22.

Elfenbeinküste | Gipfel AU und EU in Abidjan | Conde
Mwenyekiti wa AU anayeondoka madarakani rais wa Guinea Alpha CondePicha: Reuters/L. Gnago

Viongozi  wa  mataifa  55  wanachama  wa  Umoja  wa  Afrika watakutana  kujadili  njia  za  kuimarisha  hali  ya  maisha  barani  Afrika na  kuufanyia  mageuzi  Umoja  wa  Afrika ili kwamba  uwe  katika nafasi  nzuri  ya  kufanikisha  malengo  muhimu.  Viongozi  wa  Afrika tayari  mwaka  jana  walikubaliana  kuufanyia  mageuzi  Umoja  huo.

Chombo  hicho  cha  bara  la  Afrika  kinakabiliwa  na  matatizo  ya fedha  na  kukosa  uwezo  wa  kugharamia  operesheni  zake  za kulinda  amani. Bado ni  tegemezi  kwa  misaada  ya  kifedha  kutoka nje. Mwaka  2015 , asilimia  75 ya  bajeti  yake ya  uendeshaji  ilitoka kwa  wafadhili  wa  kimataifa, kama  Marekani  na  Umoja  wa  Ulaya.

Wakosoaji

Wakosoaji  pia  wanadai  kwamba  Umoja  huo  umekuwa  ukiburuza miguu  mno  kuchukua  hatua  dhidi  ya  hatari  za  kiusalama.

Somalia Mogadischu | AMISOM-Fahrzeug
Operesheni za kulinda amani katika bara la AfrikaPicha: DW/S. Petersmann

Rais  wa  Rwanda  Paul Kagame  anaongoza  juhudi za  mageuzi. Julai mwaka  jana , alichaguliwa  kuchukua  nafasi  ya  rais  wa  Guinea Alpha Conde  kuwa  mwenyekiti  wa  AU. Rwanda  imechukua  wadhifa wa uenyekiti  wa  Umoja  wa  Afrika  mwanzoni  mwa  mwaka  2018. Mapendekezo  ya  mabadiliko  tayari  yako  mezani. Kwa  mujibu  wa Kagame , nguzo  kuu  ya  mageuzi  ya  AU yanapaswa  kuwa  ni  uwezo wa  kujigharamia.

"Ni hatari  kwa  Afrika  kutegemea  kwa  kiasi  kikubwa  vyanzo  vya fedha  ambavyo  kuna  uwezekano  mkubwa  wa  kukauka  haraka kuliko  hapo  baadaye,  hususan  wakati  tuna  uwezo  wa  kulipia mipango  ambayo  ina  faida  kwetu," aliandika  Kagame  katika  taarifa iliyochapishwa  katika  gazeti  la  New Times  mjini  Rwanda wiki  hii.

"Ni  muhimu kuendeleza  misingi  na dhamira  ambayo  inahamasisha kuleta  mageuzi, wakati  huo  huo kuonesha  uwezo  wa  kubadilika katika  masuala  fulani  ambako  mataifa  wanachama  wanataka," Kagame  aliongeza.

UN Mission UNAMID
Wanajeshi wa Umoja wa mataifa pamoja na Umoja wa Afrika wakishirikiana katika jimbo la Darfur , SudanPicha: picture-alliance/dpa/S. Price

Yann Bedzigui , mtafiti  katika  taasisi  ya  mitaala  ya  kiusalama  mjini Addis Ababa  pia  anafikiri  kwamba  Umoja  wa  Afrika  unapaswa kuendeleza  msukumo  huo  wa  hivi  sasa. "Tunapaswa  kuendelea  ili kuweza  kuleta  athari  ya  muda  mrefu," alikiambia  kituo cha matangazo  cha  DW. Bedzigui  anahisi  kwamba  AU tayari  imekwisha piga  hatua  kubwa  ikilinganishwa  na  mtangulizi  wake, Umoja  wa nchi  za Afrika  OAU.

Utekelezaji  wa  hatua za  mageuzi

"Kiasi  ya  theluthi  mbili  ya  fedha  zinatoka  kwa  wafadhili, hivi  sasa wanapaswa  wao  wenyewe  kufanyakazi  ili  kuweza  kuongeza michango  ya  mataifa  ya  Afrika.

Hatua  fulani  zimekwisha  pigwa  katika  nyanja  hii. Mataifa wanachama  yamekubaliana  kuhusiana  na  pendekezo  la  kugharamia Umoja wa Afrika  kwa  michango  ya  asilimia  0.2  ya  kodi  zitokanazo na  bidhaa  zitakazoingizwa  katika  mataifa  hayo   kuanzia Julai  mwaka jana.

Mataifa  20 wanachama  yametia  saini  kwa ajili  ya  mfumo  huu  na nchi  14  zimo  njiani  kuutekeleza.

Kwa mujibu  wa  Alex Vines , mkurugenzi wa  mpango  wa  Afrika  katika taasisi  ya  kukusanya mawazo  ya  Chatham House, kuna  tatazo  la kuelewana, kwa  sababu  baadhi  ya  jumuiya  za  kanda, kama ECOWAS tayari  zinatekeleza  kodi  ya  kuingiza  bidhaa  kutoka   nje  ili kugharamia  shughuli  zao. Hii  huenda  ikawa na  maana  mataifa  ya Afrika  magharibi  hayatakuwa  na  hamasa  ya  kupandisha  kodi  hiyo.

Versammlung der Afrikanischen Union - 30 teilnehmende afrikanische Nationen
Bendera za mataifa ya Afrika katika mkutano huoPicha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Vines  anahisi kwamba  kuna  mapendekezo mazuri  kwa  mageuzi  ya AU mezani, lakini  masuali  juu  ya  utekelezaji  bado  yanaendelea kuwako.

Mwandishi: Schwikowski, Martin / ZR /  Sekione Kitojo

Mhariri: Daniel Gakuba