1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika waanza leo Addis Ababa

30 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CzXa

Umoja wa Afrika unaanza mkutano wake wa kilele mjini Addis Ababa Ethiopia hii leo.

Mkutano huo unalenga kuuongezea nguvu uwezo wa umoja huo kusuluhisha mizozo kama vile mzozo wa Darfur na Somalia.

Tangu kuundwa kwake mnamo mwaka wa 2002, Umoja wa Afrika umekabiliwa na tatizo la ukosefu wa fedha na ari ya kisiasa kuchukua hatua muafaka katika maeneo tete barani Afrika.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, anahudhuria mkutano huo baada ya kukamilisha ziara ya siku moja mjini Kigali, Rwanda.

Kiongozi huyo aliyatembelea makumbusho ya mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka wa 1994 na kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo, Paul Kagame.

Ban Ki Moon amesema ataujadili mzozo wa kisiasa nchini Kenya pamoja na viongozi wa Afrika kutafuta ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika kukabiliana na mgogoro huo.

Wakati huo huo, rais wa Libya, Muammar Gaddafi, amesema viongozi wa Afrika wanaokutana mjini Addis Ababa wanapaswa wakome kupoteza muda na waungane kuunda serikali ya Umoja wa Afrika kuyazuia mataifa ya kigeni kulitawala bara hilo.