1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika

Hamidou, Oumilkher1 Februari 2008

Viongozi wa Afrika wasihi mizozo ifumbuliwe kwa amani

https://p.dw.com/p/D0qD
Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Alpha Oumar KonarePicha: picture-alliance/ dpa


Mizozo nchini Kenya ,Darfour na kati ya Sudan na Tchad imegubika mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.


Kimsingi mkutano huu wa kilele uliopewa jina"maendeleo ya kiviwanda barani Afrika,ulilengwa kuyashughulikia

masuala ya kiuchumi .Lakini mizozo ya kila aina na hasa machafuko ya umwagaji damu nchini Kenya,mvutano kati ya Sudan na Tchad ,Somalia na pia katika visiwa vya Komoro imegubika mijadala tangu jana mjini Addis Ababa.


Miito na nasaha zimetolewa na viongozi mbali mbali wanaohudhuria mkutano huo unaoendelea hadi jumapili ijayo.


 Katibu kuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare wamewasihi wakenya wasake njia za amani kuufumbua mzozo wao.Mwito na nasaha kama hizo zimetolewa pia kwa viongozi wa Sudan na Tchad wajizuwie katika mzozo wao wa mpakani ili kutohatarisha juhudi za amani za Darfour.


"Hali inatisha na inaweza kuzidisha makali ya mzozo wa Darfour-Amani inabidi ipatikane kote nchini Sudan" amesema katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,katika hotuba yake mbele ya viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.


Mwenyekiti mpya wa umoja wa Afrika,rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amesema mara baada ya kuchaguliwa  bara la Afrika linabidi lijishughulishe wenyewe na mustakbal wake na sio kutegemea nchi za nje.


"Tunaona haya baadhi ya wakati kusikia kila kwa mara watu wanazungumzia mizozo ya bara la Afrika.Tunabidi tukiri,hili ni jukumu letu wenyewe"amesema rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi mara baada ya kuchaguliwa na viongozi wenzake 53.


Rais Kikwete ambae nchi yake ni jirani na Kenya na ana uhusiano mzuri na viongozi wa Nairobi,ambako pia juhudi za amani za Umoja wa Afrika zimeshika kasi ,ameshika nafasi ya rais John Kufour wa Ghana.


Nchi za eneo hilo zimeichagua Tanzania dhidi ya Sudan inayolaumiwa na mashirika ya haki za binaadam na baadhi ya jumuia za kimataifa kwa kuzidi kupalilia mzozo wa Darfour.


Akihutubia mkutano huo ,rais wa Umoja wa visiwa vya Comoro,Ahmed Abdallah Sambi ametangaza azma yake ya kuingilia kijeshi haraka iwezekanavyo, ili kama anavyosema "kurejesha mamlaka ya taifa na kumaliza mzozo wa kisiwa cha Nzuwani unaodumu tangu miezi kadhaa iliyopita."


Viongozi wa mataifa 53 ya Umoja wa Afrika wanatazamiwa pia kumchagua mwenyekiti wa halmashauri ya umoja huo,atakaeshika nafasi itakayoachwa na bwana Alpha Oumar Konare.

►◄