1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa juu ya Afrika:Kikwete asema ni wa mafanikio

Abdulrahman, Mohamed23 Septemba 2008

Nchi tajiri zatakiwa kutimiza ahadi yao ya 2005 kuongeza maradufu msaada kwa bara hilo .

https://p.dw.com/p/FNIE
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.Picha: AP Photo

Mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa juu ya maendeleo ya Afrika umemalizika jana,pakitolewa wito kuzitaka nchi tajiri ziheshimu ahadi zilizotoa kuongeza maradufu msaada wao wa kila mwaka kwa bara hilo, linalopigania kufikia lengo lake la kupunguza kiwango cha umasikini ifikapo 2015. Mkutano huo umefanyika kandoni mwa kikao cha mwaka cha baraza kuu la umoja huo mjini New York.

Waakilishi wa zaidi ya nchi 160 walilipitisha kwa maridhiano azimio la kisiasa kuhusu mahitaji ya maendeleo ya Afrika. Azimio hilo linasema " Tuna wasi wasi kwamba kwa hali ya sasa, ahadi ya kuongeza maradufu msaada kwa Afrika ifikapo 2010, kama ilivyofafanuliwa katika mkutano wa kilele wa mataifa tajiri ya kundi la G8 mjini Gleneagles (Scotland) haiwezi kufikiwa."

Likaongeza," Tunatoa wito wa kukamilishwa ahadi ya msaada rasmi wa maendeleo unaofungamana na ahadi hizo, ikiwa ni pamoja na ahadi ya mataifa mengi yalioendelea kufikia lengo la 0.7 asili mia ya pato jumla la taifa kwa ajili ya msaada rasmi wa maendeleo ifikapo 2015."

Katika mkutano wa Gleneagles, mataifa yalioendelea kiwanda ya kundi la G8-Marekani, Japan, ujerumani, Ufaransa, Uingereza,Italia, Canada na Urusi yaliahidi kuimarisha msaada kwa Afrika

Viongozi hao wapatao 40 waliokutana katika mkesha wa mjadala wa kila mwaka wa baraza kuu la umoja wa mataifa,ni pamoja na Rais Nikolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya na wenzao kadhaa kutoka bara la Afrika, akiwemo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

Azimio lao pia linatoa wito kwa nchi za kiafrika na jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano ili kukipa msukumo kilimo endelevu na maendeleo ya vijijini, pamoja na kusisitiza juu ya umuhimu wa usalama wa chakula.

Rais Kikwete akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika alilikaribisha azimio hilo pamoja na uwazi wa majadiliano ya pande hizo mbili, yaliofanyika siku tatu kabla ya mkutano wa kilele mjini New York juu ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia kote duniani. Kikwete alitamka " Ilikua siku ya mafanikio kwa Afrika."

Viongozi wa Afrika walisisitiza kwamba mzozo wa fedha unaozikumba nchi zilizopiga hatua kiuchumi, usiwe sababu ya kujitenga na ahadi yao ya kuimarisha msaada kwa bara hilo.

Mnamo mwaka 2000 mkutano wa dunia ulikubaliana juu ya kutimizwa kwa malengo manane ya milenia na nchi zote ifikapo 2015. Hayo ni pamoja na kupunguza kwa nusu idadi ya watu wanaoishi katika umasikini .

Aidha katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon pia aliyataka mataifa tajiri yatekeleze ahadi ya mkutano wa Gleneagles 2005, kuongeza maradufu msaada kwa Afrika na kufikia dola 50 bilioni.

Wakati huo huo Rais Sarkozy aliwaonya wafadhili wapya kama vile China dhidi ya kile alichokiita kuchochea" mzozo mpya wa madeni" kwa Afrika.

Sambamba na hayo wachambuzi wa nchi za magharibi wamekua wakionya kwamba hatua ya China kuzipa serikali za kiafrika mabilioni ya dola kama msaada usio na masharti na mikopo rahisi, inaweza kuzirejesha nchi hizo katika madeni wakati ni karibuni tu zilipatiwa nafuu au hata baadhi kufutiwa madeni hayo. Wanahoji kwamba mtindo huo wa China unahujumu juhudi za kushajiisha na kuimarisha demokrasia na utawala bora.