1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Bruxelles

Oumilkher Hamidou29 Oktoba 2010

Pendekezo la Ujerumani na ufaransa la kutaka mkataba wa Lisbon ufanyiwe marekebisho limekubaliwa kwa sehemu tuu

https://p.dw.com/p/Ps61
Kansela Angela Merkel (kati,kulia)pamoja na viongozi wenzake wa Umoja wa UlayaPicha: AP

Usalama wa sarafu ya pamoja ya Euro ndio iliyokuwa mada kuu mnamo siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya ulioanza jana mjini Bruxelles.Mabishano na misimamo inayotofautiana ndiyo iliyohanikiza mazungumzo kuhusu kufanyiwa marekebisho mkataba wa kuhakikisha utlivu wa sarafu ya pamoja Euro.Chanzo cha mabishano ni pendekezo la kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa la kutaka mkataba wa Lisbon ulioanza kutumika tangu december mwaka 2009 ufanyiwe marekebisho.Hatimae lakini maridhiano yaliweza kupatikana.

Hali ingeweza kuwa nyengine,lakini alfajiri ya leo kansela Angela Merkel alikuwa na ripoti ya kutia moyo.Madai yake yaliyokuwa yakibishwa kutaka mkataba wa Lisbon ufanyiwe marekebisho ili kudhamini utulivu wa sarafu ya pamoja Euro yamekubaliwa kwa sehemu.

"Wote walikuwa wanakubaliana kwamba panahitajika utaratibu wa kudumu wa kukabiliana na migogoro pindi ikitokea.Na wote walikuwa wanakubaliana kwamba huu ni utaratibu unaobidi kuanzishwa na nchi wanachama na wote walikuwa wanakubaliana kwamba mkataba unahitaji kufanyiwa marekebisho kidogo." Amesema kansela Angela Merkel.

Marekebisho hayo yatakuwa ya aina gani,jibu litapatikana katika mkutano mwengine wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika December mwaka huu.

Mkataba huo ulioidhinishwa kwa shida na Ireland na jamhuri ya Tcheki umeanza kutumika tangu mwaka mmoja tuu uliopita.Ukifanyiwa marekebisho itamaanisha nchi zote 27 zitalazimika tena kuuidhinisha.

Na hata kama viongozi wa Umoja wa Ulaya wanataraji hapatakuwa na haja ya kuitishwa kura ya maoni ya wananchi kwakua marekebisho hayo si makubwa,hata hivyo wanatambua pia kwamba mtihani unaweza pia kutokea.

Flash-Galerie EU Mitglieder Fahnen
Bendera za nchi 27 wanachama wa Umoja wa UlayaPicha: AP

Pendekezo la pili la kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kutaka mwanachama yeyote wa zoni ya Euro atakaekiuka masharti ya kuhakikisha utulivu wa sarafu ya Euro apokonywe haki ya kupiga kura katika baraza la mawaziri halijapita.Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,José Manuel Barroso amesema kuwapokonya wanachama haki ya kupiga kura" si jambo linalokubalika wala kutekelezeka."

Hata hivyo viongozi wa taifa na serikali wamekubaliana rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy afanye uchunguzi kuhusu wale ambao nakisi za bajeti zao zinapindukia kiwango kilichowekwa.

Mwandishi:Henn Susanne/Hamidou Oummilkheir

Mpitiaji:Yusuf Saumu Ramadhan