1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

--

Nina Markgraf5 Februari 2010

Mkutano huo unawakusanya maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi na kidiplomasia kutoka sehemu mbalimbali duniani.

https://p.dw.com/p/LtwU
Waziri wa nchi za nje wa China Yang Jiechi atakayeufungua mkutano huo .Picha: AP

Mkutano wa kimataifa juu ya usalama, unafunguliwa jioni hii  katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Munich,  huku mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa China na Iran wakiwa ni miongoni mwa watakaoshiriki katika mkutano huo ambao unawakusanya kiasi ya  maafisa  300 wa  ngazi ya juu wa kijeshi, diplomasia na  wanasiasa kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Mkutano huo wa  usalama mjini Munich ambapo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Yang Jiechi na mwenzake wa Iran Manouacher Mottaki watahutubia, unatajwa kama "Davos ya sera ya usalama " baada ya lile jukwaa la kiuchumi duniani lililofanyika mwezi uliopita  katika mji wa mlimani nchini Uswisi.

Mkutano huo wa siku tatu unafuatia siku kadhaa za kuzorota haraka uhusiano wa Marekani na China  pamoja na ishara kutoka Iran kwamba huenda ikalikubali pendekezo la nchi za Magharibi kutuma madini ya Uranium nchi za nje ili kurutubishwa.

Hali hiyo inaweza kwa kiasi fulani kuondoa wasi wasi kwamba Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za kinuklea. Marekani imemtaka rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran atowe pendekezo madhubuti kwa shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa.

Mkuu wa  mkutano huo wa Munich Wolfgang Ischinger aliiambia televisheni ya umma ARD kwamba amefurahi kuona Iran inatuma ujumbe wa   wa ngazi ya juu.

Kwa upande wa China, uungaji wake mkono utahitajika katika kuishinikiza Iran, lakini   China imekasirishwa na  hatua ya Marekani ya kufikia mkataba wa kuiuzia silaha Taiwan  ambayo China inaichukulia kuwa ni sehemu yake na pia tangazo la  Marekani la uwezekano wa Rais Obama kukutana na  kiongozi wa dini ya Budha wa Tibet Dalai Lama ikulu mjini Washington baadae mwezi huu. China inasema Dalai Lama ni  mtu hatari anayepigania kujitenga kwa jimbo hilo la Tibet.

Wakati hutuba ya waziri wa nje wa China ikiwa  ni miongoni mwa zile zinazosubiriwa kwa  makini,Waandalizi wa mkutano huo wa  kimataifa juu ya usalama  wa kila mwaka , ukiwa wa 46 , wanataka pia kuzingatia  ukuaji wa uchumi wa Asia na umuhimu wake katika jukwaa la kimataifa .

India na Pakistan zinatuma pia  wajumbe wa ngazi ya juu katika mkutano huo wa usalama wa Munich. Marekani itawakilishwa na  Seneta John Kerry, mshauri wa usalama wa taifa James Jones na mjumbe maalum anayehusika na Afghanistan na Pakistan Richard Holbrooke.

Wengine wanaotarajiwa ni Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov na  rais hamid Karzai wa Afghanistan.

Miongoni mwa  mada kuu ni uhusiano kati ya Urusi na Marekani na pia wajumbe wanatarajiwa kugusia mkutano wa mwezi uliopita  kuhusu Afghanistan mjini London , matarajio ya siku za usoni ya Umoja wa kujihami wa NATO  na mizozo inayotokana  vyanzo vya maji  na matumizi yake pamoja na  mali asili nyengine.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Josephat Charo