1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujinga na umaskini ndio chanzo cha itikadi kali

30 Julai 2015

Zaidi ya wajumbe 500 kutoka nchi zaidi ya 20 wanahudhuria mkutano kuhusu dini ya kiislam katika mji mkuu wa Senegal Dakar. Lengo la mkutano huo ni kuirejeshea hadhi yake dini ya kiislam .

https://p.dw.com/p/1G7LC
Msahafu mkongwe kabisa uliokuwa umehifadhiwa katika chuo kikuu cha BirminghamPicha: picture-alliance/dpa/Birmingham University

Mkutano huo wa kimataifa unaosimamiwa na rais Macky Sall wa Senegal na mfalme Mohammed wa tano wa Moroko umeitishwa kutokana na juhudi za jumuia ya kiislam Jamhiyatou Ansarud-Din (JAD) iliyobuniwa katika miaka ya 40 na kiongozi wa zamani wa kidini wa Senegal Baye Nias.Jumuia hiyo imeenea katika nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Nigeria.

Mchango wa dini ya kiislam katika kupatikana amani ya kudumu ndio mada kuu katika mkutano huo wa siku mbili wa Dakar."Amani ndio kipa umbele cha enzi hizi,alisisitiza rais Macky Sall alipofungua mkutano huo akisema amani inamhusu kila mtu.Na kama alivyosema Imam Ibrahima Dieng,dini ya kiislam haiwezi kukaa kimya katika ujenzi wa dunia ya amani na maendeleo."Tunaona tangu muda sasa kuna watu wanaojificha nyuma ya dini ya kiislam kuandaa mashambulio na kuwauwa waislam wenzao kwa kutumia jina la dini ya kiislam,katika wakati ambapo Mtume Muhammad anahimiza amani.Kwa hivyo dini ya kiislam inahimiza amani,inapigania amani na si chochote chengine badala ya amani."

Ujinga,Umaskini na ukosefu wa haki ndio chanzo cha itikadi kali

Mojawapo ya sababu za itikadi kali katika dunia ni ujinga na kukosa kuielewa ipasavyo dini ya kiislam amesema Murtallah Busoeri wa chuo kikuu cha jimbo la Lagos nchini Nigeria.Anautaja mfano wa Nigeria ambako sawa na katika nchi tatu nyengine za ziwa Chad-Cameroon,Chad na Niger,wafuasi wa itikadi kali wa kundi la kigaidi la Boko Haram wanazidi kufanya mashambulio wakiwatumia watu wanaoyatoa mhanga maisha yao.

Nigeria Anschlag in Gombe
Shambulio la Boko Haram mjini Gombe nchini NMigeriaPicha: picture-alliance/dpa

Ujinga ndio chanzo kikuu cha itikadi kali anashadidia pia Mohammed El Hanefi Dehah,mhadhiri wa historia na ustaarabu wa kiislam katika chuo kikuu cha Nouaktchpott nchini Mauritania."Watu wanavutiwa na dini ya kiislam lakini hawajui kwamba hilo ndilo linalowafanya wafanye vitendo ambavyo vimepigwa marufuku na dini ya kiislam.

Vijana wa kiislam wamehudhuria kwa wingi katika mkutano huo kuhusu dini ya kiislam:"Amani ya kimsingi ni jukumu la vijana na kizazi kinachokuja.Dini ya kiislam tutairejeshea hadi yake kwa kufuata ujumbe wa amani tu.Kwa hivyo hilo ndilo litakalokuwa jukumu la kimsingi la vijana. Ikiwa wataelimika, na ikiwa watafuata mwongozo wa dini ya kiislam kule hasa uliko,hakuna atakaeweza kuwahadaa na kuwaingiza katika makundi ya kigaidi,makundi yanayokinzana na mwongozo wa dini ya kiislam."

Mbali na ujinga,umaskini na ukosefu wa haki ni miongoni mwa sababu zinazowafanya vijana wadanganyike na kujiunga na makundi ya kigaidi wataalam mkutanoni wanasema.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba