1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

310309 UNFCC Klima Konferenz

Charo Josephat/ Quaile 31 Machi 2009

Njia ya kuelekea kwenye mkutano wa Copenhagen Denmark Disemba mwaka huu

https://p.dw.com/p/HNhn
Yvo de Boer kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mabadiliko ya hali ya hewaPicha: AP

Kufikia Aprili 8 wajumbe zaidi ya 2000 wa serikali, viwanda na kiuchumi, makundi yanayojihusisha na kuyalinda mazingira na taasisi za utafiti wanakutana mjini Bonn Ujerumani kwa mkutano wa kimataifa unaojadili mabadiliko ya hali ya hewa. Wanataka kutayarisha mkataba mpya wa kimataifa utakaochukua nafasi ya mkataba wa Kyoto abmao mamlaka yake inamalizika mwaka 2012. Mkataba huo unatakiwa kusainiwa mjini Copenhagen nchini Denmark mwezi Disemba mwaka huu. Kwa mara ya kwanza Marekani inashiriki kikamilifu kwenye mazungumzo ya kutayarisha mkata huo.

Yvo de Boer, kiongozi wa sekretariati ya Umoja wa Mataifa inayohusika na maswala ya hali ya hewa, ana matumaini makubwa kwamba jumuiya ya kimataifa mwaka huu itafikia makubaliano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

"Kuna maoni tofauti kuhusu lini utoaji wa gesi za viwandani duniani unatakiwa kufikia kiwango chake, na kwa kiwango gani unatakiwa kupungua kufikia katikati ya karne na mambo gani nchi zinatakiwa kufanya kuhusu vipimo vya mwaka 2020. Lakini jambo muhimu kwangu ni kufikia makubaliano ya kisiasa mwezi Disemba mwaka huu kuhusu vipi mabadiliko ya hali ya hewa yatakavyokabiliwa katika ngazi ya kimataifa."

Kwa de Boer bado kuna muda wa kuweza kuendelea kupunguza utoaji wa gesi za viwandani ili kuzuia kuongezeka kwa kiwango cha ujoto na kukizuia kibakie chini ya nyuzi 2. Hili lakini litawezekana tu wakati makubaliano yatakapofikiwa kwenye mkutano utakaofanyika mjini Copenhagen nchini Denmark mwezi Disemba mwaka huu.

Anju Sharma ni mshauri wa maswala ya hali ya hewa wa shirika lisilo la kiserikali la Oxfam nchini Uingereza. Anaona kuna mapungufu miongoni mwa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani linapokuja swala la kuchukua hatua mahsusi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Nadhani kwa mashauriano kuendelea mbele na ili kuwepo kuamiana miongoni mwa nchi mbalimbali, ahadi nyingi zilizotolewa lazima zitimizwe. Jambo muhimu ni kutoa fedha na nadhani ni muhimu wakati huu nchi zilizoendelea zitoe fedha kuonyesha zinataka kweli kuchukua hatua."

Hata kuhusu takwimu za ongezeko la ujoto, shirika la Oxfam na mashirika mengine ya kimataifa yana wasiwasi. Kiongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maswala ya hali ya hewa anaeleza lengo la Umoja wa Ulaya kupunguza gesi za viwandani kwa asilimia 20 kufikia mwaka 2020 au kwa asilimia 30, ikiwa nchi nyingine ziko tayari kushiriki, kuwa cha juu mno. Kwa Anju Sharma na mtandao wa kimataifa wa hali ya hewa, Climate Action Network, anasema kiwango hicho ni kikubwa mno.

Wael Hmaidan anauwakilisha muungano wa hali hewa wa nchi za kiarabu kwenye mkutano wa Bonn. Huu ni muungano unaoyajumulisha mashirika yasiyo ya kiserikali. Ana matumaini kwamba nchi zinazoendelea zitasimama kidete kwa umoja katika mazungumzo yanayoendelea kwenye mkutano wa Bonn na zitakuwa na ujasiri zaidi linapokuja swala la kuzinyoshea kidole cha lawama nchi zilizoendelea kiviwanda kuhusu tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa. Pia angetaka kuwe na lengo la pamoja la kupunguza utoaji wa gesi ya "carbon dioxide" katika nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kiwango maalum.

"Itakuwa vigumu kwenye mazungumzo haya kuwasilisha takwimu, kwa sababu itahitaji mchakato wa kisiasa katika nchi zao kuidhinisha takwimu maalum. Tumekuwa tukisubiri kwa mwaka mmoja na miezi mitatu kupata kupata takwimu hizo na imebakia miezi minane na bado hatujazipata. Sasa tunahitaji nchi zinazoendelea ziwe jasiri na ziwasilishe takwimu zao maalum kufikia mwaka 2020."

Anju Sharma wa shirika la Oxfam anahofu kwamba hakuna nchi yoyote iliyoendelea kiviwanda inayotaka kutoa ahadi. Hakuna serikali iliyotayari kuachana na masilahi yake ya kitaifa. Wengi wana matumaini makubwa kwamba kwa kuwa Marekani chini ya rais Barack Obama, inashiriki katika mazungumzo ya mabadiliko ya haliy a hewa, sasa inaweza kuchukua jukumu la kuongoza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Lakini Anju Sharma anaonya juu ya kuwa na matumaini makubwa.

"Kuna matarajio makubwa kwamba Marekani huenda ikafanya mengi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa lakini nadhani tunapawa kuelewa kwamba rais Obama anakabiliwa na shikizo kubwa nchini Marekani."

Wanaharakati wa mazingira wamezitaka nchi zilizoendelea kiviwanda kama Urusi, Japan na Canada ziwasilishe viwango maalumu vya kupunguza utoaji wa gesi za viwandani. Lakini pia nchi zinazoiunukia haraka kiuchumi kama vile China na India ni ufunguo muhimu katika kufikia makubaliano ya kimataifa yatakayochukua nafasi ya mkataba wa Kyoto kwenye mkutano wa mjini Copenhagen nchini Denmark mwezi Disemba mwaka huu.


Mwandishi: Quaile, Irene/ Charo

Mhariri: Abdul-Rahman