1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi - Davos

M.Knigge - (P.Martin)28 Januari 2009

Zaidi ya viongozi 40 wa nchi na serikali na zaidi ya wanauchumi 1,400 kutoka mataifa 90 wanahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi mjini Davos, Uswisi chini ya kivuli cha mzozo wa fedha ulioathiri ulimwengu mzima.

https://p.dw.com/p/GhsD
An overhead view is seen of the congress center at the World Economic Forum in Davos, Switzerland on Tuesday Jan. 27, 2009. Business participants will spend the week searching for solutions to the financial crisis with some 40 world leaders, but without the top finance officials of the new U.S. administration who are occupied by the crisis or by the confirmation process at home. (AP Photo/Michel Euler)
Kituo cha Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi katika milima ya Alps nchini Uswisi.Picha: AP

Viongozi wa kimataifa na mamia ya wanauchumi wakikusanyika kwa mkutano wa Davos wa kila mwaka, mada kuu inayozungumzwa ni hali ya uchumi duniani inayozidi kuwa mbaya.Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao na Vladimir Putin wa Urusi watatoa hotuba za kufungua mkutano huo wa siku tano ambako viongozi wengi wanatafuta njia za kuchangamsha haraka uchumi unaodorora. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na mawaziri wakuu Gordon Brown wa Uingereza na Taro Aso wa Japan waliotumia mabilioni ya dola kukabiliana na mzozo wa fedha ni miongoni mwa viongozi 40 wa dola na serikali watakaohotubia mkutano huo.

Baadhi ya nchi pia zitautumia mkutano wa Davos kupata msaada. Kwa mfano, Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatazamia kukutana na wakuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, katika jitahada ya kuondosha tofauti zilizopo kuhusu mkopo wa kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na mzozo wa fedha.Lakini mawaziri wa fedha na mameneja wa Benki Kuu na mashirika ya biashara watakuwa na majadiliano yao wenyewe wakati serikali zikijaribu kuupanga upya mfumo wa fedha.Mkutano wa Davos hauhudhuriwi na afisa wa ngazi ya juu kutoka Marekani,licha ya kuwepo matumaini makubwa kuwa serikali mpya ya Marekani itachangia sana kufufua uchumi.

Kwa upande mwingine, makundi yanayopinga utandawazi yanasema, waliokusanyika Davos kutafuta suluhisho kwa mzozo wa fedha ni wale wale waliosababisha mzozo huo.Alexis Passadakis wa kundi mojawapo linalopinga utandawazi amesema:

"Watu hao watajaribu kupata ufumbuzi - na mzigo wa gharama hizo watapachikwa raia wa kawaida,ambao hata wakati wa neema waliteseka chini ya mfumo wa uchumi uliokuwepo hivi sasa"

Kuna hofu kuwa nchi zinazoendelea na zile zilizo masikini zitazidi kuathirika kutokana na mzozo wa fedha,wakati viongozi wa nchi tajiri wakitumia mabilioni ya dola kuimarisha uchumi nchini mwao. Kwa mfano, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika,Donald Kaberuka alipozungumza pembezoni mwa mkutano wa Davos alisema,mipango mbali mbali ya misaada katika nchi tajiri humaanisha kuwa Bara la Afrika huenda lisipate msaada ulioahidiwa hadi mwaka 2010 na madola tajiri. Bill Gates mwenyekiti wa zamani wa kampuni ya kompyuta Microsoft, amepanga kutoa mwito wa kufanywa jitahada mpya kuwasaidia masikini.