1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kuinua uchumi

Oumilkher Hamidou12 Januari 2009

Mzozo wa gesi,mzozo wa Mashariki ya kati na mkakati mpya wa kuinua uchumi

https://p.dw.com/p/GWQS
Kansela Angela MerkelPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamechambua zaidi mvutano wa gesi kati ya Urusi na Ukraine na mzozo wa Mashariki ya kati. Lakini tutupie jicho zaidi kilichoandikwa na SÜDDEUTSCHE ZEITUNG kuhusu mkutano wa leo hii wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano  kuhusu mkakati wa pili wa kuinua uchumi.   



Kitakachotokana na mkutano huo ni mpango utakaoziridhisha pande zote; Kwa sababu kila upande unataka kuwaridhisha walio wake. Serikali itataka kutumia fedha nyingi ili kupunguza michango ya bima ya afya, kama wanavyotaka SPD, au kurekebisha malipo ya kodi za mapato, kama wanavyotaka wana CDU/CSU. Yote hayo lakini hayatasaidia kitu na wala wananchi hawatahisi kitu. Wakati huo huo, washirika katika serikali kuu ya muungano watawekeza fedha kidogo tuu shuleni, katika vyuo vikuu, ujenzi wa barabara na miundo mbinu mengineyo ya maana. Vitega uchumi vitahimiza ukuaji wa kiuchumi na kuendelea kukua haraka baadaye. Kwa vyovyote vile mkakati huu wa serikali utabainisha ni wa maana. Yuro bilioni 50 zitatosha kuzuwia uchumi usidorore."



Maoni ya kutia moyo yameandikwa pia na mhariri wa gazeti la WEST DEUTSCHE ALLGEMEINE linalochapishwa mjini Essen.


Kwa mtazamo jumla, mtu anaweza kusema kitita hicho cha fedha kitakachotolewa leo na serikali kuu ya muungano ni cha maana. Fedha zaidi kugharimia shule na barabara zilizojaa mashimo, malipo kidogo tuu ya kodi na hasa kwa watu ambao mishahara yao ni haba, viwango vya chini vya malipo ya bima ya afya-yote hayo yatasaidia kuinua uchumi unaoelekea kulegalega. Na hakuna atakayedai baadaye kwamba serikali kuu imefanya uzembe. Uchumi unaporejea nyuma kwa asilimia mbili na serikali inapotia njiani mkakati unaofikia asilimia moja nukta tano ya pato jumla la ndani ili kuinua shughuli za kiuchumi, hapo mtu anaweza kusema serikali haikupakata mikono."


Kuhusu mzozo wa gesi kati ya Urusi na Ukraine, gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin linaandika:


Pengine siku tatu kutoka sasa, pale gesi ya kutoka Urusi itakapoanza upya kuelekea katika nchi za Ulaya kupita mabomba ya Ukraine, na wakaazi wa eneo la Balkan kuacha kutetemeka kwa baridi, mzozo huu utatoweka magazetinmi na katika vyombo vyengine vya habari. Lakini kuamini kwamba na mzozo kati ya Moscow na Kiev utakua nao pia umeshamalizika, ni sawa na kujihadaa tuu. Mpaka sasa bado makampuni ya Gazprom la Urusi na Naftogas la Ukraine yanazozana kuhusu bei ya gesi na kiwango cha fedha Urusi inayobidi kulipa kwa gesi yake kupitia katika ardhi ya Ukraine. Kilicho dhahiri ni kwamba Ukraine iliyodhoofishwa sana na mzozo wa fedha haitaweza kumudu hata nyongeza ya wastani ya bei ya gesi ya Urusi.