1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kutafakari njia ya kumaliza umwagaji damu ana vurugu nchini Irak mjini Sharm -el-Sheikh

Mohammed Abdul-Rahman2 Mei 2007

Huu ni mkutano wa pili wenye lengo hilo katika muda wa miezi miwili,

https://p.dw.com/p/CHEy
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice (kushoto)akiwa na mwenzake Misri Ahmed Aboul Gheit wa Misri.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice (kushoto)akiwa na mwenzake Misri Ahmed Aboul Gheit wa Misri.Picha: AP

Maafisa wa kibalozi wa ngazi ya juu kutoka sehemu mbali mbali duniani wanakutana katika mji wa Sharm el-Sheikh nchini Misri leo, kujaribu kutoa msukumo mkubwa wa kidiplomasia, kwa lengo la kuutatua mzozo wa Irak, ulioanza kwa uvamizi wa 2003 ulioongozwa na Marekani na Uingereza.

Wakati kukiwa na matumaini kwamba mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yanaweza yakasaidia kumaliza umwagaji damu, pia kumekuweko na uvumi juu ya nafasi ya kuweza kukutana wajumbe wa Marekani na Iran kandoni mwa mkutano huo-ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka 30.

Akiwa njiani kuelekea Misri, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema kwamba ni jukumu la majirani wa Irak kuonyesha nia ya kutaka kumaliza matumizi ya nguvu na mauaji huko Irak, akionya kuwa utulivu wao wenyewe umo hatarini.

Bibi Rice aliwaambia waandishi habari kwamba “ Risala muhimu kabisa ambayo nitaiwasilisha ni kuwa Irak yenye utulivu, ilioungana na ya kidemokrasi, ni Irak itakayokua nguzo ya utulivu katika Mashariki ya kati, na kwamba Irak isiyo na utulivu na isiyo ya watu wote, itageuka kuwa chanzo cha ukosefu wa utulivu kwa eneo hilo.”

Katika kile kinachoonekana kuwa mageuzi katika sera ya Marekani, Rice akitarajiwa kuzungumza na wajumbe wa Syria na Iran, nchi ambazo zimeshutumiwa na Marekani kuwa Syria inawafadhili wanamgambo wa Kissuni na Iran wale Kishia, katika harakati za kuivuruga Irak.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema wakati akizungumza na waandishi habari aliposimama huko Ireland, kwamba atakua tayari kuyajadili masuala mengine mbali na hali ya Irak atakapokutana na waziri mwenzake wa Iran, ikiwa ni pamoja na mgogoro kuhusu mpango wa kinukleya wa Iran.

Hata hivyo naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mehdi Mostavafi alisema jana kwamba bado wakati si muwafaka kuzungumza na Marekani.

Katika kikao cha mashauriano huko Sharm –el-Sheikh leo, msemaji wa serikali ya Irak Ali al-Dabbagh aliitaka jamii ya kimataifa isaidie kuinusuru nchi yake. Wakati mkutano wa mawaziri 27 wa kigeni na wajumbe wengine 22 ukisubiriwa kuanza , Misri imeweka ulinzi mkali na Bibi Rice anayetarajiwa kuwasili baadae leo, anapanga kukutana mara moja kwanza na Waziri mkuu wa Irak Nuri al-Maliki na maafisa wengine.

Mkutano huo unafanyika wakati huko Marekani, Wademokrats wanajaribu karata nyengine leo, katika muswada wa kutaka paweko na ratiba maalum ya kuondoka kwa majeshi ya Marekani nchini Irak. Lakini tayari Rais Bush amejizatiti kuupinga kama alivyoupinga jana kwa kura ya turufu, ule muswada wa kutaka kuzuwia fedha za kugharimia harakati za jeshi hilo huko Irak