1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kwanza kati ya Obama na Netanyahu

Oumilkher Hamidou19 Mei 2009

Wahariri na wadadisi wa Israel wachambua mazungumzo kati ya Obama na Netanyahu

https://p.dw.com/p/HtVi
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais Barack Obama wa Marekani

Hitilafu za maoni zilizojitokeza wakati wa mazungumzo ya kwanza kabisa kati ya rais Barack Obama wa Marekani na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,mjini Washington zimezusha hofu nchini Israel,ambako wadadisi wanahofia uhusiano pamoja na mshirika huyo wa jadi usije ukapooza.


"Wamekubaliana wasikubaliane."Baada ya saa tatu za mazungumzo,hawajakubaliana juu ya jambo lolote"-limeandika gazeti la Yediot Ahronot-linalosomwa na wengi nchini Israel.

"Sijawahi kuona mazungumzo rasmi kumalizika mjini Washington huku hitilafu za maoni zikijitokeza wazi wazi kama hivi" amesema kwa upande wake Akiva Eldar,mtaalam wa masuala ya kisiasa ambae pia ni mhariri wa gazeti la Haaretz anaeishi tangu miaka kadhaa sasa mjini Washington.

"Mtu anaweza kuagulia nini viongozi hao wawili wamezungumzia ana kwa ana kwa muda wa saa moja na nusu"-ameongezea.

Akihojiwa na shirika la habari la Ufaransa-AFP,Eytan Gilboa,professor wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Bar-Ilan cha mjini Tel-Aviv ,ambae pia ni mtaalam wa siasa za Marekani,anahisi enzi mpya imechomoza katika uhusiano kati ya Israel na Washington.

Kwa maoni yake,"rais mpya wa Marekani hana hisia za aina pekee kuelekea Israel.Anatetea masilahi yake na msimamo jumla kuelekea eneo lote la mashariki ya kati."

"Ikiwa Netanyahu atashikilia msimamo wake,kuna hatari ya kuzuka mvutano ambao utakua na madhara makubwa kwa Israel."Amesema professor huyo wa chuo kikuu cha Bar-Ilan cha mjini Tel Aviv.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Robert Gibbs hakubaliani na hoja kwamba mazungumzo ya rais Obama na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yaligubikwa na hisia za uhasama.

"Kama hali ilikua mbaya hivyo,na kama kweli kulikua na mada za mabishano,kwanini basi viongozi hao wawili wakazungumza dakika 30 zaidi ya vile ilivyopangwa?"

Rais Barack Obama anaetaka kufufua utaratibu jumla wa amani ya Mashariki ya kati,anajaribu kuzijongelea pia nchi za kiarabu, kwa kutoa mwito wa kuundwa dola la Palastina na anataka pia kuanzisha mazungumzo pamoja na Iran ili kuitanabahisha iachane na mradi wake wa kinuklea.

Kwa maoni ya Gerald Steinberg,mtaalam katika chuo kikuu cha Bar-Ilan,"enzi za Obama ni tofauti na zile za George W. Bush lakini uhusiano wa dhati na wa kihistoria kati ya Marekani na Israel hauwezi kutiliwa shaka.

"Tusubiri hotuba ya Obama atakayoitoa June nne ijayo mjini Cairo kuhusu mkakati jumla wa amani ya mashariki ya kati.Lakini viongozi hao wawili,Obama na Netanyahu wamezungumzia hitilafu zao za maoni,kwa lengo la kuzisawazisha na hakuna shinikizo lolote linaloikumba Israel" amesema mtaalam huyo wa masuala ya kisiasa.

Akihojiwa kwa muda mfupi na radio ya kijeshi ya Israel,waziri wa ulinzi Ehud Barack amesema pia "anaamini mkutanao wa Washington ulikua awamu ya kwanza tuu ya mdahalo."

Viongozi wa utawala wa ndani wa Palastina wameyataja matamshi ya rais Obama kuhusu umuhimu wa kuundwa dola la Palastina kua ni ya kutia moyo.Lakini wafuasi wa itikadi kali wa Hamas wanasema ni "maneno matupu tuu ambayo hawayatilii sana maanani."

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman