1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Lima wakabiliwa na shinikizo

11 Desemba 2014

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi nchini Peru, unakimbizana na muda kuweza kukamilisha makubaliano, ambayo yanaazimia kupunguza kiwango cha utoaji wa gesi inayoongeza joto duniani

https://p.dw.com/p/1E2Va
Mkutano wa mazingira unatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa mjini Lima
Mkutano wa mazingira unatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa mjini LimaPicha: picture-alliance/dpa/P. Aguilar

Wakati ikibaki siku moja tu ili mkutano huo uhitimishe kazi zake, bado kuna wasiwasi kuhusu kupatikana kwa rasimu ya mkataba ambao utatoa ramani kwa mazungumzo ya kimazingira, ambayo yanalenga kufikia makubaliano ya kihistoria katika utunzaji wa mazingira ya dunia ifikapo mwezi Desemba mwaka 2015.

Katika mkutano huo wa Lima yameibuka upya malumbano ya muda mrefu, kuhusu nchi zinazopaswa kuchukua hatua zaidi za kupungua utoaji wa hewa ya ukaa ambayo imesababisha mabadiliko makubwa ya tabia nchi.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya mazingira Miguel Arias Canate, amelalamika kwamba rasimu inayotarajiwa inazidi kuwa kubwa kimaandishi, badala ya kupewa muundo unaoeleweka kirahisi. Malalamiko yake yaliungwa mkono na kiongozi wa Ujumbe wa Marekani Todd Stern, ambaye alitoa wito kwa mchakato huo kuwa na dira inayoeleweka.

Wito wa ushirikiano

Viongozi mbali mbali walioshiriki katika ufunguzi rasmi wa kikao cha marais kwenye mkutano huo, walisisitiza umuhimu wa ushirkiano wa kila nchi katika kukamilisha ramani ya mkataba unaotarajiwa kutiwa saini mjini Paris mwaka kesho, ambao unaazimia kuweka kikomo cha ongezeko la joto ulimwenguni kwa kipimo cha nyuzi 2 za celsius ikilinganishwa na kile cha enzi za kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Rais wa Peru Ollanta Humala
Rais wa Peru Ollanta HumalaPicha: Getty Images/C. Bouronclea

Rais wa Peru Ollanta Humala alisema suala la mabadiliko ya tabia nchi halina budi kupewa umuhimu kama ule wa hatari nyingine zinazoikabili dunia.

'Nadhani umefika muda wa kulichukulia tatizo hili kwa uzito wake kama inavyofanyika dhidi ya madawa ya kulevya na ugaidi. Nadhani hili linastahili hata kipaumbele, kwa sababu madhara yake yanatishia kuiangamiza dunia nzima''. Amesema rais wa Peru.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alizialika nchi zote kutoa mchango katika kufanikisha mkutano huo wa Lima, akisema taasisi anayoiongoza itaonyesha mfano.

''Suala hilo ni lenye kipaumbele kwangu na kwa Umoja wa Mataifa. Ni matumaini yangu kwamba kila mmoja atajiunga na mchakato huu, ambao unatupeleka katika njia ya mahali ambapo heshima ya kila mtu itazingatiwa''. Amesema Ban.

Utoaji wa gesi chafu umeshutumiwa kusababisha ongezeko la joto ulimwenguni
Utoaji wa gesi chafu umeshutumiwa kusababisha ongezeko la joto ulimwenguniPicha: picture-alliance/ dpa

Kipimo cha ufanisi wa nishati endelevu

Katika mojawapo ya hatua za mafanikio katika mkutano huo wa Lima, hapo jana ulianzishwa ushirika ujulikanao kama '1 Gigaton Coalition' ambao utakuwa ukiratibu mafanikio ya miradi ya nishati endelevu katika mataifa mbali mbali, ambayo kwa wakati huu ufanisi wake haujulikani.

Muungano huo unaoungwa mkono na serikali ya Norway unatarajiwa kunusuru mabilioni ya dola yanayotumiwa kugharimia nishati inayoharibu mazingira, na wakati huo huo ukiiepusha dunia na mabilioni ya tani za hewa ya ukaa kila mwaka.

Shirika la kimataifa la Mazingira limetoa ripoti mwaka huu, inayoonyesha kwamba ikiwa nishati endelevu itafanywa chaguo lakwanza, uchumi wa dunia utapata faida ya dola trilioni 18 ifikapo mwaka 2035.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre/press release

Mhariri:Josephat Charo