1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani utakaofanyika mjini Copenhagen

22 Septemba 2009

Dhamira ya kisiasa sasa inahitajika miongoni mwa mataifa ili kuweza kuyafanikisha mazungumzo kwenye mkutano wa mjini Copenhagen juu ya suala la mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/Jm9Y
Mkuu wa sekretariat wa kitengo cha masuala ya hali ya hewa Bw. Yvo de BoerPicha: picture-alliance/ dpa

Katika makala yake mwandishi wetu Helle Jeppesen anasema kabla ya kuzungumzia juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, mabadiliko ya sera za kisiasa pia yanalazimu kufanyika.

Wajumbe kutoka kote duniani watakutana katika mji wa Copenhagen mnamo mwezi wa Desemba kuzungumzia juu ya tishio linalotokana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Mikutano mingi sana ya matayarisho imeshafanyika takriban katika kila pembe ya duniani kwa ajili ya mazungumzo hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa.Lakini kabla ya mazungumzo hayo ,viongozi wa dunia wanapaswa kufanya mabadiliko katika sera zao la sivyo mkutano wa mjini Copenhagen haitafikia lengo lake.

Logo der UN Klima Konferenz 2009 in Kopenhagen
Nembo ya Mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa mjini Copenhagen

"Ikiwa tutaendelea kwa mwendo huu kama ambavyo tumekuwa tunafanya hadi sasa, hatutafanikiwa."

Huyo ni mkuu wa sekretariat ya kitengo cha masuala ya hali ya hewa kwenye Umoja wa Mataifa Yvo de Boer. Alisisitiza hayo hivi karibuni baada ya kufanyika mkutano wa tatu wa matayarisho ya mkutano wa Copenhagen uliofanyika mjini Bonn. Bwana Yvo de Boer alivunjika moyo baada ya mkutano huo kwa sababu hakuona hatua za kusonga mbele. Jee hatua hizo zitaonekana leo kwenye mkutano mwingine wa matayarisho wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York?

Ni mambo gani yanayolazimu kufanyika ili mkataba mpya wa kimataifa juu ya hali ya hewa upitishwe mjini Copehagen utakaochukua nafasi ya mkataba wa Kyoto?

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ulinzi wa mazingira UNEP Bwana Achim Steiner amesema yapo mambo mawili yanayozuia juhudi za kuleta mafanikio.

Yapo mambo mawili ambayo ndiyo hasa yanayozuia njia ya kufikiwa kwa mkataba.

Kwanza ni vipi,nchi za viwanda zitakavyoonyesha mfano katika kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Na jambo la pili mpango wa kuaminika katika kutenga fedha, utakaozihamasisha nchi zinazoendelea nazo pia zishiriki katika juhudi hizi za kimataifa badala ya kuongoza katika njia ya peke yao. Tunafanya juhudi juu ya masuala hayo mawili katika mazungumzo.

Mabadiliko ya hali ya hewa ni tishio kubwa kwa nchi zinazoendelea. Mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha ukame,uhaba wa maji,mafuriko na maafa ya aina mbalimbali yanayotokana na athari za mabadilikio ya hali hewa.

Jee itawezekana kufikia mkataba kwenye mkutano wa Copenhagen ili kutatua matatizo kama hayo yanayozikabili nchi zinazoendelea.

Mkurugenzi wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Bwana Achim Steiner amesema watu sasa wana sababu ya kuwa na wasiwasi.

"Nafikiri Dunia ina wasiwasi kwa haki kabisa.Kwa sababu hatuoni ujasiri wa kisiasa,uongozi na utayarifu wa kuchukua hatua ya kwanza tunayohitaji ili kufikia makubaliano kwenye mkutano wa mjini Copenhagen."

Viongozi wa nchi za G/20 pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon watakuwa na fursa ya kujadili utayarifu huo mjini Pittsburgh kabla ya mkutano mwingine wa matayarisho utakaofanyika mjini Bangkok mwezi Oktoba.

Mwandishi/Jeppesen, Helle/ZA

Imetafsiriwa na / Mtullya Abdu.

Mhariri/ Othman Miraji