1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Novemba 2017

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi, mauwaji katika kanisa la Sutherland Springs Texas Marekani, na jinsi matajiri wanavyokwepa kulipa kodi za mapato ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini

https://p.dw.com/p/2nAEt
Deutschland COP23 UN Klimakonferenz in Bonn
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Tunaanzia Bonn unakoendelea mkutano wa wiki mbili wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, COP 23. Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linazungumzia jinsi mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi mjini Bonn yanavyoshawishi mazungumzo ya mjini Berlin ya kuunda serikali ya muungano kati ya vyama vya Christian Democratic Union-CDU, Christian Social Union, CSU, waliberali wa FDP na walinzi wa mazingira die Grüne. Gazeti linaendelea kuandika:" Mabadiliko yanashuhudiwa pia kwengineko. Kwasababu mkutano wa Bonn unashawishi pia mada za wawakilishi katika mazungumzo ya muungano wa Jamaica wanaojaribu kusaka njia za kuunda serikali ya muungano mjini Berlin.  Suala kwamba Ujerumani haitaweza pengine kutekeleza ahadi iliyotoa ya kupunguza kwa asili mia 40 gesi ya sumu inayotoka viwandani hadi ifikapo mwaka 2020, limejipatia umuhimu mkubwa hivi sasa. Katika wakati ambapo ulimwengu mzima uliokusanyika mjini Bonn unazungumzia namna ya kuhifadhi tabia nchi, haitakuwa vizuri kama wenyeji wa mkutano huo watapunguza viwango walivyokuwa wamejiwekea hapo awali. Na hasa katika zama hizi za Donald Trump."

 Mauwaji ya Texas na mjadala kuhusu uhuru wa kumiliki silaha

Nchini Marekani mjadala kuhusu uhuru wa kumiliki silaha unazidi kuhanikiza katika wakati ambapo wakaazi wa Texas wanaendelea kuomboleza vifo vya wapenzi wao waliouliwa kanisani jumapili iliyopita. Gazeti la "Rhein-Zeitung" la mjini Koblenz linaandika: "Hakuna kitakachobadilika katika itikadi za kumiliki silaha. Kwasababu watu hawana azma na wala hawataki kufanya mageuzi ya kweli. Ukweli huo umedhihirika kufuatia hoja za mwanasheria mkuu wa Texas aliyetoa wito baada ya mauwaji ya kanisani, silaha zaidi zipelekwe katika "nyumba za Mungu". Si hikma pale wanasiasa wanapoitumia hoja ya "uhuru wa kila raia", baada ya kila shambulio la kigaidi , lakini wanashindwa kufanya chochote licha ya ukweli kwamba pekee mwaka huu watu 13158 wameuliwa kwa kupigwa risasi. Mauwaji katika kanisa la kibaptisti la Sutherland Springs yanadhihirisha kwa jinsi gani wamarekani na hasa wazungu, wanakabiliwa na hatari ya mtutu wa bunduki ambayo ni kubwa zaidi kupita vitisho kutoka nje.

Matajiri wanazidi kusaka mbinu za kuzidi kutajirika

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na nyaraka za siri zilizofichuliwa na vyombo vya habari kuhusu mbinu za matajiri na viongozi wengine mashuhuri za kukwepa kulipa kodi za mapato-nyaraka zinazojulikkana kama "Paradise Papers. Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linaandika:"Kwa mara nyengine tena nyaraka za Paradise Papers" zinadhihirisha jinsi matajiri wakubwa wakubwa wanavyosalimisha mabilioni ya fedha na kuzificha katika zile nchi ambako hawalazimiki kulipa kodi za mapato. Hata hivyo mjadala utakuwa unafuata mkondo ambao sio ikiwa wataendelea kuwanyooshea kidole wale wanaoutumia mfumo huo. Wakuzongwa na masuala hapa ni wale waliorahisisha mfumo huo. Kimoja tu ndicho kitakachosaidia kuzifunga bustani za peponi kwa wanaokwepa kulipa kodi, nacho ni Uwazi. Na hapo wanasiasa wanabidi wawajibike kupitia kanuni na sheria . Badala ya kutoa miito tu.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman