1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya na NATO

Oumilkheir Hamidou
5 Desemba 2017

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO unaanza mjini Brussels. Mzozo wa Ukraine sawa na mradi wa nuklea wa Korea ya kaskazini ni miongoni mwa mada mkutanoni.

https://p.dw.com/p/2ons7
Belgien Federica Mogherini in Brüssel
Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/V. Mayo

 Kabla ya kuhudhuria mkutano huo wa Brussels, Sigmar Gabriel anaeongoza wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani kwa muda hadi mazungumzo ya kuunda serikali mpya yatakapokamilika,  amesema mjini Berlin Ujerumani kwa ushirikiano pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya inabidi ipiganie wenyewe masilahi yake ulimwenguni bila ya kuitegemea Marekani."Umoja wa Ulaya utanusurika tu utakapofafanua masilahi yake na kutambua nguvu zake" amesema Sigmar Gabriel.

Matamshi hayo ameyatoa kabla ya kwenda Brussels kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi wanachama wa umoja wa ulaya na wenzao wa jumuia ya kujihami ya NATO. Licha ya tofauti za maoni zilizopo pamoja na rais Donald Trump wa Marekani, Sigmar Gabriel ametetea umuhimu wa ushirikiano pamoja na Marekani. "Kila liwezekanalo linabidi lifanywe kuhakikisha hatuzidi kutengana" amesema waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani kabla ya mkutano wa Umoja wa ulaya na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson. "Kila mmoja anamhitaji mwenzake licha ya tofauti za maoni zilizozuka miezi ya hivi karibuni. 

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: Imago/photothek/F. Gärtner

Mada mazungumzoni ni pamoja na miradi ya nuklea ya Korea ya Kaskazini na Iran na hali magharibi mwa Balkan

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa umoja wa ulaya walikutana mjini Brussels kwa chakula cha mchana pamoja na waziri mwenzao wa Marekani Rex Tillerson. Kabla ya hapo waziri Tillerson alizungumza na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa Ulaya bibi Federica Mogherini aliyetilia mkazo pia umuhimu wa ushirikiano wa dhati wa pande hizo mbili. Mada katika mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na makubaliano ya mradi wa nuklea wa Iran, Korea ya Kaskazini, hali ya mashariki ya kati, hali nchini Syria na pia na hali ya mambo namna ilivyo magharibi mwa Balkan. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson amesema kwa upande wake Marekani itaendelea kuwajibika mbele ya "washirika wake wa muda mrefu."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/

Mhariri:Mohammmed Abdul-Rahman