1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mawaziri wa Nje wa Umoja wa Ulaya

27 Julai 2009

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Brussels Ubeligiji wamekubali kubadilishana data zaidi za benki na Marekani katika jitahada za kupiga vita ugadi.

https://p.dw.com/p/IyKL
EU Commissioner for Justice, Freedom, & Security Jacques Barrot holds a press conference after first day of sitting of Justice and Home Affairs Council at European headquarters in Brussels, Belgium on 2009-02-26 © by Wiktor Dabkowski
Waziri wa Sheria na Mambo ya Ndani wa Umoja wa Ulaya, Jacques Barrot.Picha: picture alliance / Photoshot

Waziri wa Sheria na Mambo ya Ndani wa Umoja wa Ulaya Jacques Barrot amesema, umoja huo upo tayari kuwaruhusu wachunguzi wa Wizara ya Fedha ya Marekani wanaopambana na ugaidi,kupata maelezo zaidi kuhusu pesa zinazosafirishwa kati ya benki na taasisi za fedha. Lakini wanasheria wa Umoja wa Ulaya na makundi ya watu binafsi wanalalamika kuwa makubaliano hayo yatamomonyoa haki za wakazi wa Ulaya kuhifidhiwa data zao. Mfumo wa kimataifa SWIFT unaotumiwa kusafirisha pesa, hivi sasa unaongozwa na compyuta zilizokuwepo nchini Marekani, lakini operesheni hizo zinatazamiwa kuhamishwa Ulaya katika jitahada ya kuhifadhi data binafsi za watumizi wake.

Vita dhidi ya ugaidi ni mada iliyogusiwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband alipohutubia mkutano wa Brussels mapema leo hii. Amesema wakati umewadia kuzungumza na Wataliban wenye siasa za wastani na kuwapa nafasi ya kushiriki katika mchakato kisiasa nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa msemaji wa Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, kundi moja la waasi linalohusika na Taliban limeshakubali kuweka chini silaha. Hiyo ni .

Georgia ni mada nyingine iliyojadiliwa na mawaziri wa nje mjini Brussels na wamekubaliana kurefusha ujumbe wao nchini Georgia hadi Septemba 14 mwaka 2010. Tangu Oktoba mwaka jana, Umoja wa Ulaya una kikosi cha wasimamizi 200 wasio na silaha kwenye mpaka wa Georgia na majimbo ya Ossetia ya Kusini na Abkhazia yaliyojitenga na Georgia. Kikosi hicho kinasaidia kulinda usalama katika kanda hiyo.

Wasimamizi wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE waliokuwepo Abkhazia na Ossetia ya Kusini mpaka vita vya mwaka jana kati ya Georgia na Urusi , hawakuwa na budi kuondoka majimbo hayo mawili baada ya Urusi kukataa kurefusha ujumbe wao. Kwa hivyo, sasa wasimamizi wa Umoja wa Ulaya wapo Georgia tu, kituo muhimu cha kupitishia gesi na mafuta hadi Ulaya ya Magharibi.

Lakini Georgia ingependa kuwa na wasimamizi kutoka Marekani pia kuisaidia dhidi ya kile kilichoitwa kitisho cha vikosi vya Kirussi kutoka Ossetia ya Kusini na Abkhazi. Baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zina wasiwasi kuwa kuiingiza Marekani katika ujumbe wa Georgia kutazusha mvutano na Urusi - muuzaji muhimu wa gesi na mafuta kwa nchi za Umoja wa Ulaya. Hata hivyo,suala hilo lilijadiliwa licha ya kutokuwepo katika ajenda ya mkutano wa leo hii mjini Brussels.

Mwandishi: P.Martin/DPA/AP

Mhariri: M.Abdul-Rahman