1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa ulaya mjini Wiesbaden

Oummilkheir2 Machi 2007

Umoja wa ulaya wapanga kupunguza wanajeshi wake huko Bosnia

https://p.dw.com/p/CHJ0
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani F.J. Jung na mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya J. Solana
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani F.J. Jung na mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya J. SolanaPicha: AP

Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa ulaya wanakutana tangu jana mjini Wiesbaden ,magharibi ya Ujerumani kuzungumzia shughuli za kulinda amani katika eneo la Balkan-wakijiwekea matumaini makubaliano ya mzozo wa Kosovo yatapatikana na hali itaendelea kua tulivu nchini Bosnia.

Wakikutana katika kikao hicho cha siku mbili mjini Wiesbaden,mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa ulaya wamedhibitisha mpango wa kupunguzwa wanajeshi 3500 toka jumla ya wanajeshi 6500 wa kikosi cha EUFOR katika Bosnia Herzegovina.

Bila ya kutaja lini hasa wanajeshi hao watapunguzwa,waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Franz Josef Jung amesema:

“Katika awamu ya awali tutapunguza vikosi viwili vyenye wanajeshi 3500.Tutachunguza hali ya mambo namna itakavyokua.Patahitajika muda pengine hadi Agosti.Kwa awamu zitakazofuatia,nnahisi tutabidi kutilia maanani hali ya utulivu katika eneo hilo.”

Uamuzi wa kupunguzwa wanajeshi hao 3500 ulipitishwa tangu jumanne iliyopita mjini Brussels na wawakilishi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya,baada ya kutulizwa hofu za Ufaransa na Italy zilizokuia zikihofia kwamba uamuzi kama huo usije ukapitishwa pia kwa wanajeshi wa umoja wa Ulaya waliko Kosovo.

Muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya Javier Solana amesema mkutanoni mjini Wiesbaden,tunanukuu “hali nchini Bosnia ni nzuri kupita kiasi na usalama umeimarika,hata kama kisiasa bado kuna mengi ya kufanya” Mwisho wa kumnukuu muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya Javier Solana.

Hali nchini Bosnia na katika eneo zima la magharibi la Balkan,itategemea ufumbuzi wa mzozo wa Kosovo,amesisitiza waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani-mwenyekiti wa mkutano huo wa Wiesbaden.Nchi za umoja wa ulaya zinaunga mkono mazungumzo ya Vienna yanayooongozwa na mjumbe wa umoja wa mataifa Martti Ahtisaari kati ya wawakilishi wa serikali ya Belgrade na Pristina.Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung ameendelea kusema:

“Tunazitaka pande hizo mbili zifikie maridhiano,kwasababu hiyo ndiyo njia pekee ya kupatikana amani ya kudumu na utulivu katika eneo hilo.Tumetilia mkazo umuhimu wa msimamo wa Ulaya katika suala hilo kwasababu,ufumbuzi ukipatikana katika suala la kanuni za siku za mbele za Kosovo,Umoja wa ulaya utawajibika katika kutia njiani taasisi za utawala unaofuata sheria, na kusimamia shughuli za polisi.”

Ufumbuzi wa Kosovo ukipatikana Umoja wa ulaya umepangiwa kushika nafasi ya tume ya Umoja wa mataifa ya kulinda amani katika jimbo hilo la Serbia lenye wakaazi wengi wenye asili ya Albania.

Mada nyengine zinazojadiliwa katika mkutano huo wa Wiesbaden ni kuhusu Afghanistan na ushirikiano pamoja na Umoja wa mataifa,Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO na Urusi.