1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutoka Munich kwenda Munich

Arnd Riekmann9 Februari 2015

Mkutano wa usalama wa Munich uliomalizika siku ya Jumapili ungekuwa fursa muhimu ya kuutatua mgogoro wa Ukraine - Lakini kama ilivyokuwa huko nyuma, mkutano huo umekuwa ishara ya mgawiko - anasema Christian Trippe.

https://p.dw.com/p/1EY9x
Deutschland Symbolbild München Unwetter
Picha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Je, Urusi inao mkakati wa muda mrefu? Au rais Vladimir Putin anachukuwa hatua kivyake ili kufikia lengo lake la kuirudisha Urusi kuwa taifa lenye nguvu tena duniani? Swali hili limekuwa likiulizwa na wanasiasa na wachambuzi kwa mwaka mmoja sasa, tangu Vladimir Putin alivyoutikisa msingi wa utaratibu wa Ulaya, kwa kuiteka rasi ya Crimea kutoka Ukraine, na kisha akaendelea kuanzisha vita mchanganyiko katika mkoa wa Donbas mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi ni mgeni anaekaribishwa katika mkutano wa Munich. Miongoni mwa watu wenye nguvu katika utawala wa Kremlin, yeye peke ndiye anaendelea kufanya mawasiliano na mataifa ya magharibi, na hivyo ameweza kutuliza migogoro kadhaa ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini uwepo wake mjini Munich mara hii ulisababisha bumbuwazi, kutikisa vichwa na vicheko. Wakati mwingine Lavrov alionekana kama vile anakariri misitari, alitumia propaganda za ufedhuli, ambazo zilitoa tafsiri kuwa mataifa ya magharibi ndiyo ya kulaumiwa, kwa sababu mataifa hayo yamekuwa na desturi ya kuivunjia heshima Urusi tangu kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti.

01.2012 DW Europa aktuell Moderator Christian Trippe
Mwandishi wa DW Christian Trippe.Picha: DW

Jukwaa la uchochezi

Tafsiri ya dhana hii ni kwamba, kila inachokifanya Urusi ni jitihada za kufuta fedheha hii ya zaidi ya miongo miwili, na hivyo kina uhalali. Matamshi ya hasira ya Lavrov kwamba mataifa ya magharibi yanafanya kama vile yalishinda vita baridi baada ya kuvunjika kwa ukuta wa Berlin yalifichua hasa dhana hiyo.

Mara nyingi hali ya kujidanganya katika siasa inapelekea kutia chumvi uwezo wa mtu na matokeo yake ni uzembe. Mwaka 2007, mkuu wa Lavrov aliutumia mkutano wa usalama wa Munich kama jukwa la uchochezi. VladImir Putin aliishambulia Marekani na jumuiya ya NATO miaka minane iliyopita - bila sababu yoyote, kama wengi walivyochukulia wakati huo.

Ukiangalia nyuma sasa, inabainika wazi kwamba kukataa kwa Putin, kwa dunia isiyo na ushindani lilikuwa ni pingamizi tu lililoelekezwa kwa mataifa ya magharibi. Kilikuwa tu kitangulizi cha sera ijayo ya kigeni ya Urusi: Nchini Georgia, Maldova, katika rasi ya Crimea na mashariki mwa Ukraine. Kuhudhuria kwa Lavrov mwaka huu ndiyo kilikuwa kitu cha kumalizia.

Mzozo mpya wa Mashariki - Magharibi

Wanahistoria wa wakati ujao watakapoulizwa wapi na lini vita mpya baridi vilikoanzia, wataunyooshea kidole mji mkuu wa jimbo la Bavaria. Munich inawakilisha mzozo mpya kati ya mashariki na magharibi, ambao unafanana na ya zamani kwa kiasi fulani. Tofauti ni kwamba safari hii katika magharibi hakuna anaeutaka mzozo huo, ambao unakosa umbo la kiitikadi. Urusi haina ruwaza mbadala ya kijamii. Jaribio la kupinga maadili ya kimagharibi kwa yale ya imani ya orthodox ya Urusi linaonekana kama juhudi isiyo na mashiko.

Uongozi wa kisiasa wa Urusi unafanya mambo kinyume na maslahi ya nchi hiyo, kwa kuziweka kando hoja za busara na badala yake kuendekeza siasa za madaraka. Hapa ndipo kumbukumbu ya mkutano mwingine wa Munich inapokuja - Mkukano wa mwaka 1938. Mataifa ya magharibi wakati huo yalidhani yangemfurahisha Hitler kwa kumgawia eneo la Sudentenland bila hata kuiuliza Jamhuri ya Check, ambayo eneo hilo lilikuwa sehemu yake.

Munich hii na inachokisimamia ndiyo hali mbaya zaidi inayoweza kuitokea Ukraine: Hiki ndicho kinachoweza kutokea pale taifa linapogeuka mpira katika mchezo kati ya mataifa yenye nguvu. Angalau rais wa Ukraine Petro Poroshenko atakuwepo pia mezani wakati Ujerumani, Ufaransa, Ukraine na Urusi zikikutana mjini Minsk siku ya Jumatano kujadili usitishaji mpya wa mapigano nchini Ukraine.

Vyoyote watakavyokubaliana - haitomaliza mzozo mpya kati ya mashariki na magharibi. Kwa hili, mvurugano ambao Urusi imeuanzisha mjini Munich tayari umekuwa mkubwa.

Mwandishi: Christina Trippe
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba