1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa NATO waanza Brussels

Mjahida 5 Februari 2015

Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanakutana hii leo mjini Brussels kujadili suala la kuundwa kikosi cha wanajeshi kitakachopambana na kitisho cha Urusi katika mgogoro wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1EVto
Mawaziri wa Ulinzi, kutoka Uingereza Michael Fallon, Ujerumani Ursula von der Leyen, Georgia Mindia Janelidze na Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Mawaziri wa Ulinzi, kutoka Uingereza Michael Fallon, Ujerumani Ursula von der Leyen, Georgia Mindia Janelidze na Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: AFP/Getty Images/J. Thys

Kulingana na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, nia ya muungano wa kikosi cha ulinzi ni kujibu uchokozi wa Urusi ndani ya ardhi ya Ukraine na pia kupamabana changamoto zinazotolewa na kundi la wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu.

Stoltenberg amesema mkutano wa leo utazungumzia pia uimarishwaji wa kikosi hicho kutoka wanajeshi 13,000 hadi wanajeshi 30,000. Ameongeza uamuzi wao unaweka wazi kwamba NATO inajitahidi kuwalinda washirika wake wote dhidi ya kitisho cha aina yoyote kutoka upande wowote.

"Kila tunachokifanya linapokuja suala la kuongeza ulizi wetu wa pamoja kwa kuimarisha kikosi cha kujibu mashambulizi cha NATO, ni cha kujilinda. Ni kujibu kile ambacho tumekiona kutoka Urusi kwa kipindi kirefu na hatua hii inaendana na majukumu yetu ya Kimataifa," alisema Jens Stoltenberg.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami NATO Jens StoltenbergPicha: AFP/Getty Images/J. Thys

Wiki iliopita Katibu Mkuu huyo wa NATO alisema mpango wa kuundwa kwa kikosi hicho cha ulinzi ni mpango mkubwa wa pamoja tangu kumalizika kwa vita baridi.

Waziri Kerry awasili Kiev kwa mazungumzo na rais Poroshenko

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amewasili mjini Kiev hii leo kwa mazungumzo na rais Petro Poroshenko pamoja na viongozi wengine wa serikali juu ya mzozo unaozidi kutokota nchini Ukraine.

Kerry anatarajiwa pia kuzungumzia uwezekano wa Marekani kutoa silaha kwa wanajeshi wa Ukraine. Aidha ziara ya Waziri Kerry inakuja huku kukiwa na shinikizo kutoka jamii ya Kimataifa ya kusitishwa kwa mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa nchi hiyo yaliosababisha watu kadhaa kuuwawa kutokana na waasi hao kusonga mbele katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali.

Awali rais Poroshenko alisema matukio ya hivi karibuni yanapaswa kuifanya NATO kutoa msaada zaidi kwa Ukraine, ukiwemo kuwapa silaha za kisasa ili wajilinde dhidi ya mapambano ya uchokozi.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: Reuters

Hata hivyo Ashton Carter anayetarajiwa kuthibitishwa hivi karibuni kama Waziri wa ulinzi wa Marekani amesema anaunga mkono mpango wa Ukraine kupewa silaha na Marekani jambo ambalo utawala wa nchi hiyo umeondoa uwezekano wa kufanya hivyo.

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden aliliambia gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung, kwamba wamesema tangu zamani kwamba hakutakuwepo na msaada wowote wa kijeshi katika mgogoro wa Ukraine.

Ukraine pamoja na washirika wake wa Magharibi wanadai Urusi inawasaidia waasi wanaotaka kujitenga kwa kuwapa silaha na kuuchochea zaidi mgogoro huo, madai ambayo Urusi inaendelea kukanusha.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri Josephat Charo