1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa nishati ya nuklia Paris

9 Machi 2010

Rais Sarkozy ahimiza matumizi ya nishati ya nuklia.

https://p.dw.com/p/MNl3
Rais Sarkozy (kushoto)Picha: AP

Akiufungua mkutano wa nishati ya nyuklia mjini Paris, Ufaransa, hapo jana, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, ameyataka mashirika ya fedha ya kimataifa kusaidia nchi zenye kiu cha nishati kuendeleza nishati ya kinyuklia. Akatangaza kuwa Ufaransa, itasaidia kueneza ufundi wa teknolojia ya nguvu za atomiki.Israel, inayosemekana kumiliki silaha za nyuklia Mashariki ya Kati, lakini haitaki kuungama hayo,inatazamiwa leo kutangaza huko Paris kwenye mkutano huu wa siku mbili kuwa inaomba msaada wa Ufaransa kutengeneza kinu cha nishati ya nyuklia kwa mradi wa pamoja na jirani yake Jordan.

Rais Sarkozy aliuambia mkutano huu wa siku mbili juu ya nishati ya nyuklia mjini Paris ,jana kuwa haelewi kwanini nishati ya nyuklia inapewa kisogo na mashirika ya fedha ulimwenguni na akaitaka Banki Kuu ya Dunia na Banki kuu ya Ulaya ya kusaidia Ujenzi Mpya na Maendeleo na mashirika mengine kuchangia zaidi.

Katika hotuba hiyo mbele ya mkutano huu ulioandaliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo,rais huyo wa Ufaransa, alitangaza kuundwa halmashauri itakayo jumuisha waalimu bora kabisa wa kifaransa na wataalamu wa utafiti wa kisayansi ili kutoa mafunzo katika sekta ya teknolojia ya kinyuklia. Akaongeza kusema kuwa, shule hiyo ya kifaransa itakuwa ndio shina la mtandao wa kimataifa wa taasisi, ikianza kwa kituo chake nchini Jordan.Ufaransa, inazalisha kiasi cha 75% ya mahitaji yake ya nishati kupitia vinu vya nyuklia kuliko nchi nyengine yoyote ya kiviwanda, na imefanya biashara ya kuunza nje ufundi wake wa vinu vya nyuklia kuwa bidhaa muhimu ya kuuza nje.

Israel, inatazamiwa leo kutangaza kuomba msaada wa Ufaransa, kuunda kinu cha nishati ya nyuklia. Waziri wake, Uzi Lindau, anatazamiwa leo kuuwambia mkutano huu wa Paris, kuwa mradi huo ni wa pamoja na jirani yake Jordan, huku Ufaransa, ikiusimamia na kutoa teknolojia yake.

Israel, haikufunga mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia na imeapa kutotia saini mapatano ya kulifanya eneo la Mashariki ya Kati huru na silaha za nyuklia- mradi ambao unahimizwa na Marekani.

Hatahivyo, Israel inaripotiwa na wengi kumiliki silaha za nyuklia, ingawa haitaki kuungama hayo.Kiroja cha mambo, ikishirikiana na Marekani, Israel iko usoni kabisa kuitisha vikwazo vikali dhidi ya Iran, ili kuuzima kabisa mradi wake wa kinyuklia ambao Israel na washirika wake wanadai inapanga kuunda silaha za nuklia.

Iran inakanusha hayo.Makamo-rais wa Marekani, Joe Biden, aliewasili leo Jeruselem, kwa mazungumzo na Israel, anaripotiwa ana azma ya kuinasihi Israel, isiishambulie Iran na kuachia kwanza vikwazo kuuma.

Wakati Ufaransa, inashikilia kuwa mkutano huu wa siku mbili unaomalizika leo si maonesho ya biashara ya kuvipigia debe vinu vyake vya kinyuklia, viwanda vya nyuklia vya Ufaransa, vilipata pigo karibuni vilipopoteza mradi wa dala bilioni 20 wa kuijengea vinu vya nyuklia Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates) uliokwenda kwa kampuni la KEPCO la Korea ya kusini, kwa vile, gharama zake zilikua nafuu zaidi.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Miraji Othman