1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Obama na Medwedew kufufua uhusiano mpya kati ya Urusi na Marekani

Thelma Mwadzaya1 Aprili 2009

Rais Obama baadaye mchana huu atakutana Rais Dmitri Medwedew wa Urusi kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa wakuu wa nchi za kundi la G20, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana.

https://p.dw.com/p/HO97
Rais Barack Obama anayejiandaa kukutana na rais wa Urusi hii leoPicha: AP


Mkutano wa viongozi hao ni ishara ya mwanzo mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo, hata hivyo lakini kunahitajika miezi kadhaa ijayo ya majadiliano magumu kati ya Moscow na Washington.


Tofauti na utawala wa Bush, ambapo uhusiano kati ya nchi mbili hizo kuwa mbaya, uongozi wa Rais Obama umeanza kuchukua hatua za kurejesha uhusiano mzuri.Na hayo aliyafanya Waziri Mpya wa Nje wa Marekani Hillary Clinton katika mkutano wake wa kwanza na Waziri mwenziye wa Nje wa Urusi Sergej Lawrow mwanzoni mwezi March huko Geneva Uswis, ambapo alisema´´Kulikuwa na majadiliano ya wazi katika maeneo ambayo bado hatukubaliani.Kile tunachohitaji ni uaminifu zaidi, utabiri na maendeleo.Na hivi vyote vinapatikana kwa kufanyakazi pamoja.´´


Miongoni mwa masuala magumu sana katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili zenye nguvu za kinuklia,ni mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami barani Ulaya.


Urusi inaona kuwa kitendo cha Marekani kuweka makombora hayo katika nchi za Jamuhuri ya Czech na Poland ni kitendo cha uchokozi dhidi yake, lakini Marekani inasema kuwa ni kwa ajili ya kujilinda na uwezekano wa mashambulizi kutoka kwa nchi kama vile Iran.


Hata hivyo tofauti na mtangulizi wake, serikali ya Obama iko tayari kufikia muafaka juu ya suala hilo kwa njia ya majadiliano.Hii inaweza ikawa ni pamoja na kuishirikisha katika utengenezaji wa mfumo wa makombora hayo.


Suala lingine nyeti ni kufikiwa kwa mkataba unaomalizika Decemba wa udhibiti wa kiwango cha silaha za nuklia.


Mkataba huo ulifikiwa mwaka 1991 na marais wa zamani wa nchi hizo Gorbachev wa Urusi na George Bush na ulikuwa msingi wa kuweko kwa udhibiti wa kiwango cha umilikaji wa silaha za nuklia.


Awamu ya pili ya makubaliano hayo ilishindwa kutekelezwa kutokana na pingamizi la mabunge ya nchi hizo, Congress la Marekani na Duma la Urusi.

Kwa mujibu wa takwimu za mwisho zilizotolewa Julai mwaka jana Marekani inamiliki vichwa 5950 vya nuklia huku Urusi ikiwa na vichwa 4100.


Hata hivyo Rais Obama kimsingi amekwishaashiria kuwa anataka kufikia makubaliano mapya ya nukilia na Urusi.

´´Moja ya malengo yangu ni kuzuia ueneaji wa silaha za nuklia.Nadhani ni muhimu kwa Marekani kushirikiana na Urusi kuongoza njia katika suala hili na nilisema hayo nilipowasiliana na rais Medvedev wa Urusi ili ajue kuwa ni muhimu kwetu kuanza tena majadiliano ya jinsi gani tunaweza kupunguza silaha za nuklia´´.


Vyovyote itakavyokuwa, mkutano wa leo kati ya Rais Obama na Rais Medvedev jijini London ni ishara muhimu ya mwanzo katika kuelekea kwenye uhusiano mzuri katika nchi hizo mbili.

Mwandishi :Daniel Scheschkewitz/Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdulrahman

ZPR